Rais wa nchi hiyo, Jacob Zuma.PICHA|MAKTABA
Johannesburg.Chama Tawala cha Afrika Kusini,
Africa National Congress (ANC) kimekasirishwa na kuzomewa kwa Rais wa
nchi hiyo, Jacob Zuma wakati wa Ibada ya kitaifa ya heshima za mwisho
kwa rais wake wa kwanza mzalendo, Mzee Nelson Mandela.
Rais Zuma alizomewa mara kadhaa na baadhi ya
waomboleza waliofurika katika Uwanja wa Michezo wa FNB (Soccer City),
juzi Jumanne na kuhudhuriwa na mamia ya wakuu wa nchi na Serikali pamoja
na watu mashuhuri kutoka sehemu mbalimbali duniani.
Mara ya kwanza rais huyo alizomewa wakati akiingia
uwanjani hapo, huku kundi jingine la watu wanaoaminika kuwa wafuasi wa
ANC likimshangilia, hali ambayo iliendelea wakati akitambulishwa na kila
sura yake ilipoonekana kwenye televisheni kubwa zilizokuwapo uwanjani.
Hali ilikuwa mbaya zaidi wakati kiongozi huyo
aliposimama kuhutubia ambapo waliompinga walionyesha wazi kiasi cha
kusababaisha kuchelewa kuanza kwa hutuba yake.
Makamu Rais wa ANC, Cyril Ramaphosa ambaye alikuwa
mmoja wa waendeshaji shughuli hiyo ya kitaifa, mara kadhaa alijaribu
kukemea zomeazomea hiyo, lakini hakusikilizwa kwani wapo waliokuwa
wakiimba wakati hotuba za viongozi zikiendelea.
Ramaphosa zaidi ya mara tatu alisikika akikemea
kile alichokiita utovu wa nidhamu kwa baadhi ya watu waliokuwa FNB.
“Tuna wageni, hebu tusijiaibishe wenyewe na tuwe na nidhamu,” alisema na
kuongeza:
“Yeye (Mandela) alikuwa ni kada mwenye nidhamu,
kwahiyo hebu basi tumsindikize katika hali ya kuwa na nidhamu,tuonyeshe
kwamba sisi tuna nidhamu katika mazingira ya aina yoyote”.
Msemaji wa ANC,Jackson Mthembu akizungumza baada
ya ibada hiyo, alisema waliokuwa wakimzomea Zuma ambaye pia ni Rais wa
ANC “wameliaibisha taifa la Afrika Kusini”.
“Tukio hili halikuwa la kisiasa wala la siasa na
hao waliozomea wamewaangusha Waafrika Kusini waliokuwapo uwanjani na
wale waliokuwa wakifuatilia tukio hili la kihitoria kupitia vyombo vya
habari,” alisema Mthembu.
Wakati Rais Zuma akizomewa, mtangulizi wake, Thabo
Mbeki pamoja na viongozi wengine kadhaa wakiwamo naibu wake, Kgalema
Motlante, Rais wa Zimbabwe, Robet Mugabe, Rais wa Marekani Barack Obama
na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Kin Moon walikuwa wakishangiliwa
kwa nyakati toauti.
Hata hivyo, baadhi ya wananchi waliliambia gazeti hili kuwa Rais Zuma “anavuna alichopanda”.
“Zuma hana hata hadhi ya kusimama katika kivuli
cha Mandela, naamini hata Madiba alipo anafahamu kwamba alipigania uhuru
wa watu lakini wale waliofuata wakiwa watawala nchi na watu havipo
katika mioyo yao,” alisema Martin Cullen mkazi wa Soweto.
Alidai kwamba Rais Zuma amenunua nyumba yenye
thamani ya kiasi hicho cha fedha sawa na Sh360 bilioni za Tanzania
wakati mamilioni ya watoto wa nchi hiyo wanakufa kwa njaa.“ANC kimsingi
wamepoteza uhalali kwa wapigakura wao”. Janine Roberts Owen mkazi wa
Houghton alisema, hakuna njia nyingine ambayo umma inaweza kuitumia
kueleza kutofurahishwa na uongozi wa ANC zaidi ya ile waliyoitumia juzi
ya kumzomea Zuma.
Source:mwananchi
Source:mwananchi
Facebook Blogger Plugin by Kibonajoro








Post a Comment
Post a Comment