Vilio na simanzi vilitanda Jumatano
iliyopita Mwananyamala Kisiwani, jijini Dar kufuatia mtoto wa mwaka
mmoja, Rahim Rajab kufariki dunia kwa kuangukiwa na watu watatu, akiwemo
baba yake mzazi, Rajab Said..
Tukio la watu hao kumwangukia mtoto
huyo lilitokea Jumatatu iliyopita na lilisababishwa na ugomvi mkubwa wa
CD yenye nyimbo za mwanamuziki wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond’
ulioibuka ndani ya chumba cha kulala kati ya mama wa marehemu na
mpangaji mwenzake aitwaye Aisha.
Akizungumza kwa machungu kuelezea
tukio hilo, mama mzazi wa marehemu Rahim, Habiba Ally alikiri kuwa kisa
cha kifo cha mwanaye ni CD tu.Akasema:
" Kwa kweli hakuna kingine zaidi ya
CD, naamini hivyo kwa kuwa mimi sikuwa na ugomvi wowote na Aisha.
Tulikuwa tunaishi kawaida tu ukiacha mikwaruzo ya hapa na pale.”
Akaongeza: Jumamosi iliyopita, Aisha
alikuja ndani kwangu na CD zake tatu, ya Diamond, Kingwendu na ya Coast
Modern Taarab. Alipomaliza kuangalia aliziacha, akaondoka zake.
“Jumapili mimi nikaenda nazo kwa mama zote tatu kwa ajili ya kuziangalia, tulipomaliza na mimi niliziacha huko.
“Jumatatu usiku Aisha akaja kunidai,
nikamwambia zipo kwa mama. Kwa kuwa anapajua anapoishi mama, si mbali
akaenda kuzichukua zote tatu.
Ajabu aliporudi tu, akaja tena kwangu
na kusema hajapewa CD ya Diamond kitu ambacho si kweli na ndipo
ulipozuka ugomvi wote huo hadi kusababisha kifo cha mwanangu.”
Akizungumza msibani juzi, bibi wa
marehemu, Jamima Hassan alisema siku ya tukio alipigiwa simu na mkwe
wake (baba wa marehemu) akamwambia kuna ugomvi nyumbani kwake unaohusu
CD kati ya mkewe na mpangaji mwenzake ambapo bibi huyo aliamua kwenda
kutatua ugomvi huo.
“Niliondoka muda huohuo kwani huyo
Aisha alitoka kwangu kuchukua CD zake muda mfupi tu, sasa nilijiuliza ni
CD gani wanazogombania?
“Nilipofika nilikuta ugomvi umepamba
moto, baba wa mtoto na mume wa Aisha aitwaye Shaban Sangali walikuwa
wameungana kumtoa nje ya chumba Aisha bila mafanikio.
“Wakati naingia, Aisha alikuwa
akitukana matusi mazito na tulipojitahidi kumtoa nje alitusukuma kwa
nguvu. Ndipo yeye, mume wake na baba wa mtoto waliwaangukia watoto
waliokuwa wamelala kitandani,” alisema bibi huyo.
Akaendelea: Tulipowaangalia watoto
ambao ni mapacha, hali zao zilikuwa mbaya, tukaamua kwenda kwa mjumbe wa
mtaa kuripoti, akatupa barua, tukaenda Kituo cha Polisi Mwinyijuma,
pale wakatupa PF3 ya kuwapeleka Hospitali ya Mwananyamala ambako
walilazwa kwa matibabu.
Bibi huyo alisema siku iliyofuata,
Rahim alifariki dunia, ikabidi waende Polisi Oysterbay ambapo walifungua
shitaka lenye faili kwa kumbukumbu No. OB/RB/1150/2013 MAUAJI.
Watuhumiwa katika RB hiyo ni Aisha na mumewe, Sangali ambao walikamatwa na kufikishwa kituo cha polisi.
Majirani waliozungumza na mwandishi
wetu walisema wakati ugomvi kati ya Aisha na Habiba unatookea, mume wa
Habiba alikuwa anarudi kutoka kazini, akakutana na kimbembe hicho.
Walisema aliingilia kati kuamua bila
mafanikio. Wakati huo mume wa Aisha alikuwa chumbani kwake na
amefungulia muziki wa redio kwa sauti ya juu hivyo hakujua nini
kinaendelea kwenye chumba cha mpangaji mwenzake.
Ikaelezwa kuwa, kuna watu walikwenda kumgongea na kumwambia mkewe anapigwa na mume wa Habiba kwa kushirikiana na mkewe.
Ilibidi mwanaume huyo atoke mbio hadi
chumbani kwenye ugomvi ambako alikuta baba wa marehemu akijitahidi
kuwaamulia wawili hao bila mafanikio.
Habari zinasema mwanaume huyo
aliingilia kati kuongeza nguvu lakini katika hali ya kuwalemea, Aisha
aliwasukuma wote na kisha wao kuwaangukia watoto hao mapacha waliokuwa
wamelala kwenye kitanda kimoja.
Katika hali ya kusikitisha, marehemu amemuacha pacha mwenzake aitwaye Rahima Rajab ambaye ni kulwa.
Wengi wanaamini kuwa maisha ya Rahima
yangekuwa ya furaha zaidi kama Rahimu angekuwepo na kwamba
itamsononesha sana akikua na kusikia mwenzake alifariki dunia kwa ugomvi
wa mama yake na mpangaji mwenzao kisa ni CD ya nyimbo za mwanamuziki.
GPL
Facebook Blogger Plugin by Kibonajoro
Post a Comment
Post a Comment