Anachechemea huku mkono wa kushoto akiwa ameufumbata kwapani, uso umekumbwa na maumivu yanayoshindana na tabasamu hafifu analojaribu kulitoa. |
ANAFAHAMIKA zaidi kwa jina la Mzee Small, lakini jina lake halisi ni Small Wangamba.
Ana sifa nyingi, lakini iliyo kubwa ni ucheshi,
uchangamfu, ukarimu na kila aina ya bashasha. Hata hivyo kwa sasa hali
yake ni tofauti, mambo mengi yamebadilika.
Sipati shida kumpata pale nilipokusudia kumfikia
na hata ninapofika nyumbani kwake katika banda la vyumba viwili ambavyo
vimemalizwa kujengwa hivi karibuni, napokewa na msichana
anayenikaribisha katika kiti nje ya kibanda hicho.
Ujumbe unapelekwa ndani kwa Mzee Small kuwa ana
mgeni na dakika 20 baadaye mlango unafunguliwa, anachomoza mtu ambaye
sipati taabu kumfahamu kuwa ni Mzee Small, mwigizaji nguli ambaye
maradhi yamemkalisha kitako.
Anachechemea huku mkono wa kushoto akiwa
ameufumbata kwapani, uso umekumbwa na maumivu yanayoshindana na tabasamu
hafifu analojaribu kulitoa.
Hali hiyo inaakisi wimbo mmoja wa Shakila Abdallah
‘Bi. Shakila’ wenye mashairi ‘Macho yanacheka moyo unalia’. Kimsingi
Mzee Small anaumwa ingawa anajaribu kutabasamu, kinachoonekana katika
paji lake la uso ni tofauti na tabasamu hafifu analojaribu kulitoa pale
macho yetu yanapogongana na wakati wa mazungumzo anabainisha
kinachomsibu.
“Sipo vizuri, naumwa. Kwa sasa inawezekana
ikaonekana kama nina nafuu kidogo, lakini naumwa,” anasema baada ya
kunikaribisha katika chumba kimoja ambacho anakimiliki na mkewe.
Chanzo cha tatizo
Anasema tatizo lake lilimuanza Mei mwaka jana
baada ya kurudi kutoka Mwanza alikokuwa na kazi ya kutumbuiza katika
tamasha la kupambana na mauaji ya Albino. Tamasha hilo liliratibiwa na
Kituo cha Under The Same Sun .
“Nilitoka Uwanja wa Ndege (Dar es Salaam) na
kufika hapa nyumbani, nikaingia chooni moja kwa moja. Lakini wakati
natoka, nikadondoka. Nilipojitahidi kunyanyuka haikuwezekana hivyo
nikabebwa hadi chumbani,” anasema.
Anasema akiwa chumbani alijaribu kujinyanyua
akajikuta anadondoka tena, hivyo akawahishwa hospitali moja jirani na
nafuu haikupatikana.
Ikalazimika apelekwe Hospitali ya Amana jijini Dar
es Salaam ambako alilazwa siku tatu kabla ya kuhamishiwa Hospitali ya
Taifa ya Muhimbili.
Facebook Blogger Plugin by Kibonajoro
Post a Comment
Post a Comment