Wakati al-Shabaab walipotawala zaidi ya nusu ya Somalia kwa miaka
kadhaa, wazazi wengi wa Somalia walilazimishwa kufanya mipango kwa ajili
ya watoto wao wa kike kutoroka kulazimishwa kuolewa na wapiganaji wa
kikundi cha wanamgambo hao.
Wanawake wa Somalia wakitembea ndani ya
kambi ya wakimbizi ya Dolo Ado huko mashariki mwa Ethiopia. Wanawake
wengi walitoroka Somalia kwenda nchi jirani kuepuka ndoa za kulazimishwa
na wanamgambo wa al-Shabaab. [Judith Schuler/World Food Programme/AFP]
Wanawake hawa walitorokea Kenya, Uganda na Ethiopia, lakini sasa
wameanza kurejea nyumbani kadri vikosi vya Somalia na Misheni ya Umoja
wa Afrika nchini Somalia (AMISOM) vinavyochukua udhibiti wa maeneo mengi
kutoka kwa al-Shabaab..
Jijini Mogadishu, Liban Ahmed alikumbuka namna mmoja wa mabinti zake
watatu alivyolazimishwa kuolewa na mwanachama wa al-Shabaab mwaka 2009.
"Binti yangu alikuwa mdogo sana na hakuwa na utashi wa ndoa wakati
mwanachama huyo asiye mwema alimuoa kwa lazima," alisema Ahmed, mwenye
umri wa mika 45. "Alikuwa na miaka 16 na alikuwa shule darasa la saba."
"Mwanaume ambaye hakuwa ananijua mimi wala familia yangu alikuja
nyumbani, akiwa na silaha aina ya AK-47," Ahmed aliiambia Sabahi.
"Aliniambia, 'Ninataka kumuoa binti yako Zamzam na mimi ni mpiganaji wa
vita vitakatifu Abu Akram.' Nilimwita binti yangu kwa haraka na
kumuuliza kama alikuwa akimjua mwanaume huyo, lakini alipomwangalia
hakuweza kumtambua, jambo lililotutisha sote," alisema.
Ahmed alisema kuwa alihisi kutishwa lakini hata hivyo alimwambia mvamizi
huyo wa al-Shabaab kwamba asingemlazimisha binti yake kuolewa naye
pasipo hiari yake. Hili lilimkasirisha mwanamgambo huyo, ambaye wakati
huo alipata kibali cha kumkamata Ahmed kutoka katika mahakama ya
al-Shabaab huko Elasha Biyaha, kitongoji cha Mogadishu.
"Siku moja baada ya kumwambia kwamba nisingeweza kumlazimisha binti
yangu kuolewa na mwanaume asiyemtaka, aliniletea taarifa inayoniagiza
kuripoti mahakamani ndani ya saa 24," Ahmed alisema.
Kukataa kumuozesha binti yake kwa mpiganaji ilikuwa ni dhambi, mahakama
ilimwambia. "Nililazimishwa kumuozesha msichana kwa mwanaume palepale
mahakamani," alisema. "Niliambiwa kumkabidhi msichana kwa mume wake
ndani ya siku tatu; Sikupewa fursa ya kushauriana na mama wa msichana
kuhusu ndoa."
"Baada ya kumueleza mama ya Zamzam kuhusu ndoa ya kulazimisha, tulianza
kuchangisha fedha kutoka kwa ndugu na siku mbili baadaye, mke wangu,
Zamzam na wadogo zake wa kike wawili walikimbilia Uganda," alisema.
Lakini al-Shabaab walipogundua kwamba wametoroka, wanamgambo walimkamata tena Ahmed.
"Nilihukumiwa bila ya kufuata haki kutumikia kifungo cha miezi sita
jela, ambacho nilikimaliza mwaka 2010, lakini namshukuru Mungu mabinti
zangu waliepukana na mateso ya kuwa wake za magaidi," alisema, akiongeza
kwamba mahakama iliamuru mpiganaji wa al-Shabaab kumpa talaka Zamzam.
Familia ya Ahmed ilirejea Somalia mwaka 2013 na sasa wanaishi kwa amani katika wilaya ya Hodan huko Mogadishu.
"Mimi na familia yangu tuna furaha kuhusu kushindwa kwa al-Shabaab,"
alisema, akililaumu kundi hilo kwa "kuwafanya watu kukaribia kuichukia
nchi yao wenyewe" kwa sababu ya unyanyasaji ambao ilibidi waupitie chini
ya utawala wa al-Shabaab.
Mkaazi mwingine wa Mogadishu, Sadiyo Mumin mwenye umri wa miaka 55,
alieleza ni jinsi mji ulipokuwa chini ya udhibiti wa al-Shabaab
alivyoogopa mabinti zake wawili watalazimishwa kuolewa na al-Shabaab.
Aliwapeleka mabinti zake -- ambao wakati huo walikuwa na miaka 19 na 22
-- kuishi na ndugu huko Ethiopia. Mumin mwaka huu alimrejesha binti yake
nyumbani kwao wilaya ya Hodan.
"Shukrani zote kwa Mungu kwa kuwaondoa al-Shabaab na kuwaokoa mabinti
zetu," aliiambia Sabahi. "Hatuna hofu tena ya al-Shabaab kulazimisha
kuwaoa mabinti zetu kwa sababu wamesambaratika na kupata laana [ziwe juu
yao] kwa mateso yote waliyoyasababisha."
Shamso Ali, mkaazi wa Daynile, mwenye umri wa miaka 26, ni bibi wa
aliyekuwa mwanachama wa al-Shabaab. Kwa miaka mitatu, alikuwa katika
ndoa na mwanachama wa al-Shabaab bila ridhaa yake, mpaka alipokufa
katika mapigano na vikosi vya wanajeshi wa serikali mwaka 2012.
"Wakati alipokuwa ananioa, aliniambia atamwambia baba yangu kwamba
tulitaka kuoana na [alinitishia] angemuua baba yangu pamoja na mimi kama
ningekataa," alisema. "Nilisikitika sana na kuwa na hofu na nilikuwa
naogopa kwamba baba yangu angeuawa kama ningelitoroka jiji".
"Hatukuwa na njia ya kupata fedha kwa ajili yangu wala wanafamilia
wengine kutoroka, hivyo niliamua kukubali pendekezo hili kabla [hali
hiyo] haijaenea," alisema. "Ninamshukuru Mungu kwamba maisha ya giza
niliyoshirikiana na mtu niliyekuwa namwogopa hayapo tena na kwamba
sikumzalia watoto."
Ndoa za kulazimishwa 'hazina msingi katika Uislamu'
Kama ilivyokuwa kwa Ali, wasichana wengine wengi ambao walilazimishwa
kuolewa na wanachama wa al-Shabaab waliishia kuhangaika katika maisha
kama wazazi pekee wa kike, wanaotakiwa kutafuta mahitaji kwa ajili ya
watoto wao bila kuwa na msaada wa baba zao ambao waliwatelekeza kwa
kuenda vitani bila kuwapa fedha yoyote.
Aina hii ya ndoa hakiubaliki kisheria katika Uislamu bila kujali nani
anayehusika, kwa mujibu wa Sheikh Nur Barud Gurhan, mtumishi maarufu wa
dini wa Kisomali na msemaji mkuu wa Umoja wa Wanazuoni wa Kiislamu
nchini Somalia.
Alisema al-Shabaab walianza kutumia mbinu hii chini ya mwavuli wa
Uislamu tangu mwaka 2007, wakitumia fursa ya familia maskini za Kisomali
ambazo tayari zimezidiwa na hali ya matatizo na vita ambavyo vilikuwa
vinaikabili nchi hiyo kwa miaka mingi.
"Waliwachukua wanawake wengi, wakiwalazimisha kuolewa na kuwanyanyasa
ili kuwafanya wafikiri kuwa wasingeweza kumkataa kisheria mujahidina
anayepigana [kulinda] dini na nchi," aliiambia Sabahi, akiongeza kwamba
wanawake na familia ambazo walikaidi walikabiliwa na adhabu za kikatili
kutoka kwa kundi hilo.
Ushahidi kwamba malengo ya al-Shabaab hayakuwa kuendeleza ndoa za kudumu
au kuanzisha jamii yenye utulivu, wanamgambo hao pia waliwaoza wanawake
wasio wenyeji wa Somalia kwa wapiganaji wa kigeni ambao walikuwa
hawazungumzi Kisomali, wakijua hawatakuwa na uwezo wa kuwasiliana nao au
kuwa na uhusiano na wake zao katika njia yoyote ya kueleweka.
"Ndoa kama hiyo hairuhusiwi kisheria katika Uislamu; haina uzuri wowote
zaidi ya kubaka na hakuna msingi kama huo katika Uislamu," mtumishi huyo
wa dini alisema.
Chanzo: http://sabahionline.com/
Facebook Blogger Plugin by Kibonajoro
Post a Comment
Post a Comment