Dar es Salaam na Dodoma. Macho na masikio ya Watanzania leo yataelekezwa kwa Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa wakati atakapoisoma hotuba ya Bajeti Kuu ya Serikali kuanzia saa 10.00 jioni bungeni, mjini Dodoma.
Sambamba na Mgimwa, pia mawaziri wa fedha za nchi za Kenya na Uganda nao katika muda huo watasoma bajeti za nchi zao.
Waziri mpya wa Fedha wa Kenya, Henry Rotich atasoma bajeti ya kwanza ya
nchi hiyo ikiwa chini ya utawala mpya wa Rais Uhuru Kenyatta wakati ya
Uganda itasomwa na Waziri wa Fedha, Maria Kiwanuka.
Dk Mgimwa aliwaambia waandishi wa habari, Dodoma jana kuwa Serikali
imetenga kiasi cha Sh18.2 trilioni kwa ajili ya mwaka ujao wa fedha wa
2013/14.
Alisema wameweka vipaumbele kadhaa ambavyo ni nishati vijijini, miundombinu, maji na upatikanaji wa pembejeo za kilimo.
Bajeti hiyo itatanguliwa na ile ya mwelekeo wa hali ya uchumi ambayo
itasomwa asubuhi na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu),
Stephen Wassira.
Dk Mgimwa alisema wananchi hasa wa vijijini watapata huduma ya maji hasa baada ya kuongezwa Bajeti ya Wizara ya Maji.
Awali, wabunge waligomea Bajeti ya Maji ya Sh398 bilioni kabla ya
kuongezwa hadi kufikia Sh582.5 bilioni ikiwa ni ongezeko la Sh184
bilioni.
Waziri Mgimwa alisema pia kuwa suala la nishati ya umeme ni kipaumbele
kingine cha Serikali na kwamba itaisambaza katika maeneo mbalimbali
nchini na zaidi katika maeneo ya vijijini chini ya Wakala wa Nishati
Vijijini (Rea).
Alisema kipaumbele kingine ni usambazaji wa pembejeo za kilimo vijijini
ili kuwasaidia wakulima kulima mazao bora. Pia alisema katika mwaka huu
wa fedha Benki ya Wakulima itaanzishwa ili kutoa mikopo yenye unafuu ya
kilimo.
Aidha, Serikali ilikwishatangaza vipaumbele vingine ambavyo ni ujenzi wa
Bandari za Tanga, Dar es Salaam, Mtwara na Bagamoyo, reli, elimu, Mfumo
wa Teknolojia ya Mawasiliano (ICT), afya na ujasiriamali.
Endelea kusoma habari hii katika kazeti la Mwananchi
Facebook Blogger Plugin by Kibonajoro
Post a Comment
Post a Comment