Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma amesema kuwa afya ya rais wa zamani wa
taifa hilo Nelson Mandela imeanza kuimarika kidogo kutokana na matibabu
anayopewa na Madaktari wake jijini Pretoria.
Rais wa zamani wa Afrika Kusini Nelson Mandela kulia na rais wa sasa Jacob Zuma
Zuma amewaambia wabunge kuwa Mandela anayefahamika kwa jina maarufu kama
Madiba ameanza kuimarika na ni habari njema kwa raia wa nchi hiyo
ambao wamekuwa wakikumbwa na wasiwasi kutokana na afya yake kuendelea
kudorora.
Rais huyo ameongeza kuwa kila mmoja anakumbuka mchango wa Mandela ambaye
alifungwa jela miaka 27 akiwa katika harakati za kupinga ubaguzi wa
rangi nchini humo na baadaye kufanikiwa kuwa kiongozi wa kwanza mweusi
nchini humo mwaka 1994.
Kiongozi huyo wa Afrika Kusini amewataka raia wa nchi hiyo na dunia
nzima kuendelea kumwombea Mandela ili apate nafuu haraka na kuruhisiwa
kurudi nyumbani.
Familia ya Mandela imesema kuwa imeguswa mno na salamu za heri njema
zinazotumwa na watu mbalimbali duniani kumtakia kiongozi huyo wa zamani
nafuu ya haraka.
Mandela mwenye umri wa miaka 94 alilazwa hospitalini Jumamosi iliyopita
baada ya kuanza kusumbuliwa na mapafu tatizo ambalo limemsumbua kwa muda
mrefu.
Hii ni mara ya nne kuanzia mwezi Desemba mwaka uliopita kwa Mandela
ambaye atatimiza miaka 95 mwezi ujao kulazwa hospitalini na mara ya
mwisho ilikuwa mwezi Aprili mwaka huu.
Mara ya mwisho kwa Mandela kuonekana hadharini ilikuwa mwezi Julai mwaka
2010 wakati wa ufunguzi wa mashindano ya soka ya kombe la dunia nchini
humo.
Via kiswahili.rfi
Via kiswahili.rfi
Facebook Blogger Plugin by Kibonajoro
Post a Comment
Post a Comment