Akiwasilisha Rasimu ya Katiba Mpya jana, Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji
Joseph Warioba, alisema baada ya kujadiliana kwa kina katika kuchambua
maoni ya wananchi juu ya mfumo wa Muungano unaofaa, Tume imefikia uamuzi
wa kupendekeza serikali tatu, ya Shirikisho, Tanzania Bara na ya
Zanzibar.
Jaji Warioba alisema kazi ya kufikia uamuzi huo
haikuwa rahisi kwa sababu katika maoni mbalimbali yaliyotolewa na
wananchi, wapo waliokuwa wanataka Muungano wa serikali moja, serikali
nne, kuendelea na muundo wa sasa wa serikali mbili na pia walikuwako wa
Muungano wa mkataba.
“Kimsingi sheria ilitutaka kuzingatia
uwapo wa Muungano. Kwa hiyo hatukuchukua maoni ambayo yanataka kuvunja
Muungano ingawa yalikuwapo ya watu wachache,” alisema katika rasimu
aliyowasilisha kwa umahiri mkubwa na kuonyesha kugusa maeneo mengi
ambayo yanakidhi kiu ya wananchi wengi.
Alisema kabla ya
kufikia uamuzi huo, walifanya rejea ya mapendekezo na maandiko
mbalimbali, kutazama uzoefu wa mataifa mengine, lakini pia kuzingatia
mapendekezo ya Tume ya Jaji Francis Nyalali na Jaji Robert Kisanga.
Tume zote zilipendekeza kuwapo kwa Muungano wa serikali tatu.
Katika kushughulikia Muungano, Jaji Warioba pia alisema kuwa orodha ya mambo ya Muungano yamepunguzwa kutoka 22 hadi saba.
Aliorodhesha mambo saba ya Muungano ambayo ndiyo yatapelekwa kwa
wananchi ili kutolewa maamuzi, kuwa ni Katiba, Ulinzi na Usalama, Uraia
na Uhamiaji, Sarafu na Benki Kuu, Mambo ya Nje, Usajili wa Vyama vya
Siasa, Ushuru wa Bidhaa na Mapato yasiyokuwa ya kodi.
Katika
mapendekezo hayo ya kihistoria, pia muundo wa Bunge la Muungano nao
umeguswa na sasa litakuwa na viti 75 tu, kwa uwiano wa wabunge kutoka
Tanzania Bara 50 na Zanzibar 20, huku wabunge watano wakiwa ni wa
kuteuliwa na Rais kutoka kundi la walemavu.
Rasimu hii mpya
ambayo itakuwa na ibara 240 kuliko ilivyo sasa yenye ibara 152, inafuta
wabunge wa viti maalum, na badala yake kila jimbo la uchaguzi litakuwa
na wabunge wawili, mmoja mwanamume na mwingine mwanamke, hali ambayo
itasaidia kuleta usawa wa kijinsia.
Kwa maana hiyo, kama
mapendekezo hayo yatakubaliwa na wananchi kupitia kura ya maoni,
Tanzania Bara itakuwa na majimbo ya uchaguzi 25 wakati Zanzibar itakuwa
na majimbo 10 tu.
Kwa sasa Tanzania Bara ina majimbo ya
uchaguzi 189 wakati Zanzibar ni 50 ikifanya jumla ya majimbo yote kuwa
239. Pia Rais ana nafasi 10 za wabunge wa kuteuliwa.
Katika
kudhibiti nafasi za ubunge na kukuza uwajibikaji, Tume inapendekeza
wananchi kuwa na haki ya kumwita mbunge na kumuhoji ikibidi kumwondoa
kwenye nafasi yake, kitu ambacho mfumo wa sasa hauna kwani
akishachaguliwa hukaa hadi kipindi chake cha miaka mitano kimalizike
hata kama hafanyi lolote.
Udhibiti wa ubunge pia umekwenda
kwenye pendekezo la kuwa na ukomo wa ubunge ambao ni miaka 15 ambayo mtu
hataruhusiwa tena kugombea.
Tume inapendekeza kufutwa kwa
mfumo wa uchaguzi mdogo na badala yake lolote litakalotokea kwa mbunge
wa jimbo anayetokana na chama cha siasa kama ataondolewa, basi orodha ya
wanachama wengine wa chama hicho itakayowasilishwa kwa Tume Huru ya
Uchaguzi ambayo itatueua mmoja kwenye orodha hiyo kuziba nafasi hiyo
kutoka chama kilichopoteza mbunge.
Hata hivyo, Tume inapendekeza kuwa uchaguzi mdogo utafanyika tu endapo mbunge aliyepoteza nafasi yake ni mgombea binafsi.
MGOMBEA BINAFSI RUKSA
Kwa maana hiyo, Tume inapendekeza mfumo wa mgombea binafsi kuanzia ngazi ya mwenyekiti wa mtaa hadi nafasi ya rais.
Suala la mgombea binafsi limekuwa ni moja ya maeneo ambayo yamezua
mvutano nchini kwa serikali kupambana kufa kupona kuzuia kuwako kwa
fursa hiyo.
Serikali ilikwisha kushindwa kesi mara mbili juu
ya mgombea binafsi, lakini ikapambana kwanza kwa kutunga sheria ya
kuharamisha mgombea binafsi, lakini baadaye kwa kuomba rejea ya kesi
Mahakama ya Rufaa dhidi ya hukumu iliyohalalisha fursa hiyo. Kesi hiyo
kwa sasa iko katika Mahakama ya Afrika mjini Arusha.
SPIKA NA NAIBU SPIKA
Katika rasimu hiyo, Tume pia inapendekaza kuwa Spika na Naibu wake
wasiwe wabunge na wala wasiwe viongozi katika vyama vya siasa.
Katika siku za hivi karibuni kiti cha Spika kimekuwa kikilaumiwa
kuyumba kupendelea chama anachotokana nacho, hali ambayo imelifanya
Bunge kukosa usawa kwa pande zote, yaani upande wa chama tawala na ule
wa upinzani.
TUME HURU YA UCHAGUZI
Tume hiyo pia
inapendekeza kuundwa kwa Tume Huru ya Uchaguzi ambayo pia itachukua
majukumu ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa.
Rasimu
inapendekeza wajumbe wa Tume Huru ya Uchaguzi wapatikane kwa kuzingatia
sifa ambazo zitaanishwa kwenye katiba, na wanaohitaji nafasi hizo
wataomba kwa Kamati ya Uteuzi ambayo itaongozwa na Jaji Mkuu, majaji
wakuu kutoka Tanzania Bara na Zanzibar, Maspika kutoka pande mbili za
Tanzania- Baraza la Wawakilishi na Bunge na Mwenyekiti wa Tume ya Haki
za Binadamu na Utawala Bora.
Aidha, Tume inapendeleza kuwa
baada ya mchakato huo, Rais akishateua Mwenyekiti wake jina
litawasilishwa bungeni ili kuthibitishwa.
MAHAKAMA
Tume
inapendekea kuendelea na mfumo wa sasa wa kuzingatia uhuru wa mahakama,
lakini inapendeleza pia kuanzishwa kwa Mahakama ya Juu (Sprime Court of
Tanzania).
Pia ipendeleza kuwa huduma zaidi kwa maana ya
rasilimali zitolewa kwa mahakama ili itekeleze kazi zake kwa uhuru na
haraka zaidi.
MADARAKA YA RAIS
Tume inapendekeza kuendelea kuwa na Rais mtendaji ambaye anachaguliwa na wananchi kwa kura katika uchaguzi mkuu.
Pia ashinde kiti cha urais baada ya kupata kura zaidi ya asilimia 50 ya
kura zote badala ya utaratibu wa sasa wa kuwazidi wenzake kura hata
kama siyo kufikia kiasi kinachopendekezwa.
Rais anapendekezwa
kuendelea kuwa Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama; na sifa
za sasa kugombea urais kwa mujibu wa katiba ziendelee ikiwa ni pamoja
na umri uwe ni kuanzia miaka 40.
Matokeo ya uchaguzi urais sasa
itakuwa ni ruksa kuhojiwa mahakamani katika Mahakama ya Juu na ni
lazima shauri hilo liwe limesikilizwa na kufanyiwa uamuzi katika kipindi
cha siku 30 ili Rais mpya aapishwe ndani ya muda unaokubalika kikatiba.
Hata hivyo, anayetakiwa kisheria kuhoji matokeo hayo ni aliyegombea kiti hicho.
MADARAKA YA RAIS YAPUNGUZWA
Tume inapendekeza kuanzishwa kwa utaratibu wa wateule wa rais
kuthibitishwa na bunge, kuteuliwa kupitia mchakato wa taasisi na vyombo
vingine katika uteuzi. Kwa sasa ni Waziri Mkuu pekee anayethibitishwa na
Bunge.
Imependekezwa kuwa uteuzi wa mawaziri, manaibu mawaziri, jaji mkuu, naibu jaji mkuu utafanywa na Rais na Bunge kuwathibitisha.
Hata hivyo, jaji mkuu na naibu wake watateuliwa na Rais kutokana na majina yatakayopendekezwa na Tume ya Utumishi wa Mahakama.
Wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama wapitishwe na Baraza la Ulinzi na
Usalama; Katibu Mkuu Kiongozi ateuliwe na Rais, lakini athibitishwe na
Bunge; makatibu wakuu wateuliwe na Tume ya Utumishi wa Umma; mawaziri na
manaibu wao wathibitishwe na Bunge.
Kinga dhidi ya Rais
endelee kama ilivyo, isipokuwa kama Bunge litaamua linaweza kuanzisha
mashitaka dhidi ya Rais kama inavyofafanuliwa kwenye katiba ya sasa.
MAWAZIRI WAPUNGUZWA
Tume inapendeleza Katiba iweke ukomo wa idadi ya mawaziri ambayo
itakuwa ni 15 kwa kuwa tayari majukumu mengi yatakuwa yamekwisha
elekezwa kwenye serikali Tanzania Bara na Zanzibar.
CHANZO: NIPASHE
Facebook Blogger Plugin by Kibonajoro







Post a Comment
Post a Comment