Serikali imesisitiza kuwa
haitavumilia kuona baadhi ya watu wanaendelea kupanda mbegu za chuki za
kidini na kisiasa miongoni mwa Watanzania na imesisitiza kuchukua hatua
bila huruma kuzimaliza njama hizo.
Kauli hiyo ilitolewa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda jana, wakati akiahirisha Mkutano wa 11 wa Bunge hadi Agosti 27, mwaka huu.
“Nataka niwahakikishie Watanzania
kuwa serikali haitavumilia hata kidogo kuendelea kupandwa mbegu za chuki
na za kidini na kisiasa miongoni mwa Watanzania.
“Serikali itachukua hatua kali bila
huruma kuzima njama hizi mbaya dhidi ya taifa letu…vile vile, hatua kali
zitachukuliwa kwa mtu yeyote atakayebainika kuhusika bila kujali hadhi
na nafasi yake katika jamii,” alisema.
Waziri Mkuu Pinda aliwasihi viongozi
wa serikali, kisiasa, kidini na wananchi wote kwa ujumla, kila mmoja kwa
nafasi yake kuwajibika ili kuhakikisha kuwa taifa linaendelea kuwa
kisiwa cha amani na utulivu.
Aliwataka Watanzania wote
kushirikiana na vyombo vya dola katika kuwabaini wahalifu hao na kukataa
vitendo vya uvunjifu wa amani katika nchini.
“Kila mwenye taarifa za kuwezesha
kukamatwa kwa watu wanaohatarisha amani ya nchi yetu atoe taarifa kwa
Jeshi la Polisi na taarifa hizo zitafanyiwa kazi kwa umakini mkubwa na
kwa maslahi ya taifa letu,” alisema.
Alisema ziko dalili ya kuwepo kwa
vikundi vya watu wachache wasioitakia mema nchi ambavyo vinataka
kupandikiza chuki za kisiasa na kidini miongoni mwa Watanzania na kuleta
mapigano na mauaji miongoni mwao.
Alisema kwa mfano, hivi karibuni,
katika kipindi cha mwaka mmoja tu uliopita pamekuwepo na matukio ya
vurugu, fujo na uvunjifu wa amani katika maeneo mbalimbali ya Arusha,
Mwanza, Mbeya, Mtwara, Morogoro, Singida na Iringa.
Alisema hofu ya migogoro ya kidini imetokea Zanzibar, Dar es Salaam, Arusha, Mwanza na Geita.
Alisema baadhi ya matukio hayo
yamesababisha vifo na majeruhi ikimwemo, kujeruhiwa askari na wananchi,
uharibifu wa miundombinu, uharibifu wa mazingira na mali za serikali na
watu binafsi.
Alisema matukio mfululizo ya fujo,
vurugu pamoja na tukio la kulipua mabomu kanisani na hivi karibuni
katika mkutano wa hadhara huko viwanja vya Soweto katika Kata ya
Kaloleni mkoani Arusha na katika kampeni ya Chadema katika viwanja
hivyo, yamesababisha hofu kubwa kwa wananchi na hisia ya uwepo wa
tishio la kuendelea kwa vitendo vinavyoashiria ugaidi nchini.
Alisema matukio ya aina hii
yakiachiwa yaendelee, uchumi wa nchi utadorora kutokana na ushiriki
hafifu kwenye shughuli za maendeleo.
Kauli hiyo ya Waziri Mkuu
inatanguliwa na nyingine aliyoitoa pia katika kikao cha bunge
kilichomalizika ambapo alisema kwa wale wanaokadi amri halali ya Jeshi
la Polisi wapigwe tu.
“Na mimi nasema wanaokaidi amri
halali ya Jeshi la Polisi wapigwe tu, kwa sababu hakuna namna nyingine
ya kupambana na wakaidi zaidi ya kuwapiga”.
Alikuwa akijibu swali la Mbunge wa
Kilwa Kaskazini(CCM), Murtaza Mangungu aliyetaka kujua ni hatua gani
zinazochukuliwa na serikali kufuatia matukio ya vurugu za mara kwa mara
nchini.
Facebook Blogger Plugin by Kibonajoro
Post a Comment
Post a Comment