Dodoma. Zikiwa zimesalia siku mbili kabla ya Bajeti Kuu ya Serikali
kusomwa, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti na Mbunge wa Bariadi
Magharibi (CCM), Andrew Chenge amesema Serikali imeelemewa na mzigo wa
madeni.

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti na Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM), Andrew Chenge
Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa anatarajia kuwasilisha Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2013/14 keshokutwa.
Chenge alisema hayo juzi Mjini Dodoma baada wa mkutano wa majadiliano ya
namna bora ya utendaji kazi baina ya Kamati ya Bunge ya Bajeti na
kamati za Miundombinu, Ulinzi na Usalama, Mambo ya Nje, Hesabu za
Serikali (PAC) na Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC).
Alisema Serikali imeelemewa na madeni huku kila wizara ikitaka
kukamilishiwa mafungu yake ya fedha jambo ambalo linashindikana kwa kuwa
hazipo.
Kwa mujibu wa hotuba ya Kambi ya Upinzani ya Wizara ya Fedha, mpaka sasa
deni la taifa limefikia Sh21.028 trilioni bila dhamana ya Serikali kwa
mashirika ya umma na binafsi hadi kufikia Desemba 2012 na kati ya fedha
hizo, asilimia 75.97 ni deni la nje.
Hata hivyo, katika majibu ya Serikali, Waziri Mgimwa alisema Serikali
imeanza kulipa na kuanzia Julai 2012 hadi Aprili 2013, malipo ya madeni
yamefikia Sh1,666.77 bilioni na kati ya hizo, deni la nje lililolipwa ni
Sh213.57 bilioni.
“Unapoamua kuminya eneo moja kwa ajili ya kupeleka fedha eneo jingine,
hapa panapominywa wanahangaika na wao wanahitaji fedha, inatakiwa
kutafuta njia nyingine ya kupata fedha kwa ajili ya eneo hilo,” alisema
Chenge.
Mwenyekiti huyo alisema wizara zote 32 zinahitaji fedha kulingana na
bajeti wanazowasilisha bungeni wakati wizara nyingine zikihitaji fedha
zaidi ili kukamilisha mipango kwa matumizi ya kawaida na maendeleo.
“Katika vikao vyetu vya ndani, tumezungumza na kila wizara. Zina
matatizo mengi kweli... wanatutaka tuwaongezee kasma, sasa sisi siyo
Serikali, tunachokifanya kamati ni kuishauri Serikali kuelekeza fedha
eneo moja lenye mahitaji ya fedha nyingi kwa masilahi ya taifa.
“Tumeishauri Serikali kuondoa fedha maeneo kadhaa na kuitaka kutenga
fedha kwa ajili ya mipango ya maendeleo, lakini wakati mwingine, hata
hizo fedha zenyewe hakuna kwa kuwa tunachokitegemea zaidi hapa ni pato
la ndani. “Sasa watu walipe kodi. Tabia ya ukwepaji kodi inasababisha
Serikali kushindwa kukusanya mapato yake. Watu wanalalamika hakuna hiki
na hiki, lakini wananchi na taasisi mbalimbali wenyewe ndiyo hao
wanaokwepa kodi, sasa utapata wapi fedha za maendeleo?
Meghji: Bajeti ina presha
Waziri wa zamani wa Fedha, Zakhia Meghji amesema kipindi cha kuelekea
kwenye bajeti, kinakuwa cha ‘presha’ hasa ikiwa waziri hakujiandaa
kisaikolojia.
Akizungumza kwenye Viwanja vya Bunge, Dodoma jana, Meghji ambaye kwa
sasa ni Mbunge wa Kuteuliwa, alisema: “Ninajivunia, katika kipindi
changu kuanzia 2005-7 nikiwa Waziri wa kwanza wa Fedha mwanamke,
nilikuwa naona fahari, ni heshima kubwa kwangu kusimama mbele ya wabunge
kuwasilisha Bajeti.
“Nilikuwa nina hofu sana mwanzoni. Nilikuwa ninawaza jinsi ya
kuwasilisha Bajeti, wabunge wananisikiliza, Watanzania wote
wananisikiliza lakini nilichokuwa ninakifanya ni kurudia-rudia kuisoma.
“Kitu kilichokuwa kinanikwaza ni kutaja zile namba... ma-trilioni sasa
nilichokuwa ninakifanya ni kuandika pembeni na kusoma moja kwa moja bila
matatizo,” alisema huku akicheka.
Chanzo - gazeti la Mwananchi
Facebook Blogger Plugin by Kibonajoro







Post a Comment
Post a Comment