Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi CUF Maalim Seif Sharif Hamad amewataka
Wanachama na Wazanzibari kwa Ujumla kuendelea kushikamana katika
kipindi hiki cha kuitolea Maoni Rasimu ya kwanza ya Katiba ya Jamhuri ya
Muungano ili lengo la Zanzibar kuwa na Mamlaka yake kamili liweze
kufikiwa.

Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif
Hamad akiwahutubia wafuasi wa chama hicho katika mkutano wa hadhara
uliofanyika Matemwe, Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Amesema mshikamano ndio uliosaidia Rasimu hiyo kupunguza mambo ya
Muungano kutoka 22 hadi 7 na kwamba jitihada zinapaswa ziendelee katika
kujenga hoja ili Wizara ya Mambo ya Nje, Benk Kuu na Sarafu, Vyama vya
Siasa, Uraia na Ushuru wa Bidhaa kutolewa katika Mambo ya Muungano.
Maalim Seif amesema hayo wakati akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika Matemwe, Mkoa wa Kaskazini Unguja mwishoni mwa wiki.
Amesema kwa maoni yake Tume ya mabadiliko ya katiba imefanya kazi kubwa
ya kukusanya na kuchambua maoni ya wananchi na hatimaye kupata rasimu ya
awali ya katiba ambayo imezingatia baadhi ya matakwa ya wazanzibari.
Amesema pamoja na mambo mengine rasimu hiyo ya awali imezingatia kwa
makini uwepo wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo imeundwa na nchi
mbili yaani Zanzibar na Tanzania Bara na kwamba mara kwa mara Rasimu
hiyo imekuwa ikitaja washirika wa Muungano.
Mambo mengine aliyoeleza kuyakubali katika rasimu hiyo ni pamoja na
kutamka wazi kuwa masuala ya Mafuta na gesi asilia, Mikopo na biashara
za nje, Ushuru wa forodha, pamoja na elimu ya juu na baraza la mitihani
kutokuwa katika Orodha ya Mambo ya Muungano.
Hata hivyo amesema kuna mambo kadhaa yanayohitajika kurekebishwa katika
rasimu hiyo ili kufikia lengo la kuwa na Zanzibar yenye mamlaka kamili.
Ameyataja mambo hayo kuwa ni pamoja na jina la Muungano ambao kwa maoni
yake unapaswa kuitwa “Muungano wa Jamhuri za Tanzania”, tofauti na
ilivyo sasa “Jamhuri ya Muungano wa Tanzania”.
Mambo mengine aliyoeleza kutoridhishwa nayo kwenye rasimu hiyo ni pamoja
na Mambo ya nje kubakia katika orodha ya mambo ya Muungano, sarafu na
benki kuu, uraia na uhamiaji pamoja na vyama vya siasa.
“Tunataka Zanzibar iwe na uwezo wa kufanya mambo yake bila ya
kuingiliwa, kwa mfano iwe na uwezo wa kujiunga na Umoja wa Mataifa (UN),
Umoja wa Afrika (AU), pamoja na FIFA”, alieleza Maalim Seif.
Aidha amesema baadhi ya vipengele vya rasimu hiyo havikutolewa maelezo
ya kutosha, hali inayowafanya wananchi kutoelewa mantiki halisi
iliyokusudiwa, na kuiomba tume ya Mabadiliko ya Katiba kuvitolea
ufafanuzi.
Miongoni mwa vipengele hivyo ni Muundo wa Muungano ambapo amesema
zilizoungana tangu asili ni Tanganyika na Zanzibar, na kutaka Tume iweke
wazi washirika hao wa Muungano.
Hata hivyo amesema rasimu hiyo bado ina kasoro nyingi ambazo zinapaswa
kujadiliwa zaidi katika mabaraza ya katiba, ili kupata rasimu ya pili
itakayokidhi matakwa ya wananchi, kabla ya rasimu hiyo kufikishwa katika
Bunge la katiba.
Maalim Seif amefahamisha kuwa Chama cha Wananchi CUF kimeunda jopo la
wataalamu wa Sheria kwa ajili ya kuipitia na kuichambua rasimu ya katiba
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliyotolewa hivi karibuni.
Amesema jopo hilo la wataalamu litakapokamilisha kazi yake, litakuwa na
upeo mkubwa wa kuushauri uongozi wa chama hicho, ili kiweze kutoa tamko
rasmi la Chama kuhusiana na rasimu hiyo ya katiba.
Amesema bado wananchi wana fursa ya kuchangia katika rasimu hiyo kupitia
wawakilishi wao watakaoingia katika mabaraza ya katiba ambapo wananchi
watatoa uamuzi wa mwisho wakati wa kura ya maoni.
Wakati huo huo Maalim Seif amewatahadharisha wananchi kutojihusisha na
vitendo vyovyote vya vurugu na uvunjifu wa amani katika kuendelea na
mchakato huo.
Kabla ya mkutano huo, Maalim Seif alifungua baraza ya CUF ijulikanayo
kwa jina la “msimamo” au “mtendeni Namba 2” katika kijiji cha
Mfurumatonga, yenye wanachama 200.
Kwenye mkutano wa hadhara alikabidhi kadi za CUF 609 kwa wanachama wapya
walioamua kujiunga na chama hicho, huku 148 kati yao wakiwa wamerejesha
kadi za CCM.
Naye Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa CUF Taifa Salim Bimani,
aliwakumbusha wananchi kujisajili katika daftari la kudumu la wapiga
kura muda utakapofika.
Facebook Blogger Plugin by Kibonajoro







Post a Comment
Post a Comment