
Dar es Salaam. Marekani imetaja sababu nne ambazo zimemfanya Rais Barrack Obama kuijumuisha Tanzania katika ziara yake ya bara la Afrika.
Rais Obama amepanga kulitembelea bara la Afrika kuanzia Juni 26 hadi
Julai 3, mwaka huu na atazitembelea pia Senegal na Afrika Kusini.
Kiongozi huyo wa Marekani ambaye baba yake mzazi ni mzaliwa wa Kenya,
anatarajiwa kuwasili nchini Julai Mosi kwa ziara ya siku tatu. Atakuwa
Rais wa tatu wa Marekani kuitembelea Tanzania baada ya Bill Clinton
mwaka 2000 na George Bush mwaka 2008.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Balozi wa
Marekani, Alfonso Lenhardt alisema sababu ya kwanza ya Obama kuja
Tanzania ni kutokana na kuwa mfano wa utawala bora, demokrasia na
ushirikishaji wa watu wake wakati wa kufanya uamuzi unaogusa maisha yao
ya kila siku.
Alisema kuwa Tanzania ni nchi ya mfano linapokuja suala la uongozi
bora na ndiyo maana imekuwa na amani na utulivu kwa muda mrefu
ikilinganishwa na nchi nyingi za Kusini mwa Jangwa la Sahara.
“Nchi nyingi za Afrika zinazoizunguka Tanzania zimekuwa na matatizo
ya vita vya wenyewe na hata ukosefu wa utawala bora,” alisema Balozi
Lenhardt ingawa alidokeza kuwa katika siku za karibuni imekuwa
ikikabiliwa na changamoto mbalimbali kutokana na matukio ya uvunjifu wa
amani.
Balozi Lenhardt alisema sababu nyingine inayomfanya Rais Obama kuja
Tanzania ni kutokana na jitihada za Serikali ya Marekani kutengeneza
mazingira mazuri ya uwekezaji na kasi ya ukuaji wa uchumi.
“Rais Obama anakuja kuunga mkono juhudi za Watanzania katika
kutengeneza mazuri ya uwekezaji lakini bila kusahau kuwa kasi ya ukuaji
wa uchumi wa Tanzania imeivutia Serikali ya Marekani,” alisema.
Balozi Lenhardt alitaja sababu nyingine inayomleta Rais Obama kuwa ni
kuisaidia Tanzania kuendeleza fursa mbalimbali za kujiletea maendeleo.
Alisema uendelezaji huo wa fursa una lengo la kuisaidia Serikali ya Tanzania kukabiliana na tatizo la umaskini.
Alisema Marekani ni moja ya nchi zinazoongoza kwa kutoa fedha nyingi
za misaada na akisema kwa mfano, mwaka 2012 pekee ilitoa Dola 750
milioni.
Aidha, alisema nchi yake imekuwa ikitoa misaada mingi kupitia Shirika
la Millenium Challenge (MCC), ambayo imejikita zaidi katika kusaidia
sekta za umeme, maji na miundombinu.
Alisema Tanzania inaunga mkono jitihada za Serikali kujitosheleza kwa chakula na inafadhili Mkakati wa Kukuza Kilimo Kusini mwa Tanzania (SAGCOT).
Alisema Tanzania inaunga mkono jitihada za Serikali kujitosheleza kwa chakula na inafadhili Mkakati wa Kukuza Kilimo Kusini mwa Tanzania (SAGCOT).
“Tunaunga mkono mpango wa SAGCOT kupitia Mfuko wa Rais wa Marekani
unaoitwa `Feed the Future’ lengo likiwa kuifanya Tanzania kupiga hatua
katika kilimo,” alisema balozi huyo.
Sababu nyingine ya ujio wa Obama ni kuhimiza haja ya Afrika
kutayarisha viongozi wa kizazi kijacho. Ameanzisha programu ya kuandaa
viongozi wa kizazi inayoitwa `Young African Leaders Initiative’ na
Watanzania watatu, Modesta Lilian Mahiga, Masoud Salim Mohamed na Malula
Hassan Nkanyemka walishiriki katika mpango huo na kukutana na kiongozi
huyo mwaka 2010.
“Rais Obama anataka kusaidia kuandaa viongozi wa kizazi kijacho wa Afrika kusimamia vizuri rasilimali za nchi,” alisema.
Tishio la China
Akizungumzia ushindani na China kuhusiana na fursa za kuwekeza na
kuvuna rasilimali za Afrika, Balozi Leinhardt alisema hawana tatizo
lolote na hilo kwani dhamira ya Marekani ni kusaidia Tanzania kupiga
hatua katika maendeleo ya kiuchumi.
Rais wa China, Xi Jinping aliitembelea Tanzania Machi mwaka huu na
ujio wa Obama umetafsiriwa na baadhi ya watu kuwa ni ushindani wa
mataifa hayo mawili katika kusaka na kunufaika na rasilimali za Afrika.
Balozi Lenhardt alieleza imani yao ni kuwa China inadumisha urafiki
na Tanzania kwa nia ya kuisaidia kuendelea… “Sisi hatuna shida na China,
kwani tunaamini wako kwa ajili ya kusaidia. Ilimradi tu wawe na dhamira
safi katika kuwasaidia.”
Alipoulizwa kama ziara ya Rais Obama ina lengo la kusaka fursa ya
kuvuna rasilimali za Tanzania, balozi huyo aliwataka Watanzania kuacha
kuwa na wasiwasi wa kuporwa rasilimali zao.
“Watanzania ni watu wapole na wakarimu ila mna tatizo moja la kuhofia
kila jambo. Kila kitu mnachofanyiwa mnaona kuna baya linakuja. Sisi
tuna nia njema ya kuwasaidia kuendelea.”
Source:Mwananchi
Source:Mwananchi
Facebook Blogger Plugin by Kibonajoro







Post a Comment
Post a Comment