Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This


UFAFANUZI WA TAARIFA MBALIMBALI  ZILIZOTOLEWA KWENYE VYOMBO VYA HABARI DHIDI YA DAWA BANDIA YA  KUPUNGUZA MAKALI YA UKIMWI YENYE JINA LA BIASHARA TT-VIR 30 TOLEO NAMBA 0C.01.85.


Tarehe 9 Mei, 2013, Mhe. Dkt. Hussein A. Mwinyi (Mb) Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, katika kuhitimisha hoja ya bajeti  ya Wizara alitolea ufafanuzi suala la dawa bandia ya ARV kufuatia hoja  zilizokuwa  imetolewa na Mhe. Zarina S. Madabida (Mb) kuhusu kuhusika kwa  kiwanda cha dawa cha Tanzania Pharmaceutical Industries Ltd (TPI) katika sakata la dawa bandia ya ARV.
Baada ya ufafanuzi huo wa Mhe. Waziri kutolewa, kumekuwa na taarifa mbalimbali  kupitia vyombo vya habari zinazoleta mkanganyiko kwa wananchi kuhusu suala  hili.
Ili  kuondoa mkanganyiko ambao umeanza kujitokeza, Wizara inapenda kutoa ufafanuzi  kuhusu tamko lililotolewa na Mhe. Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii.
Aidha, kama ilivyoelezwa katika taarifa mbalimbali za umma zilizokwisha kutolewa na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii pamoja na TFDA  kuhusiana na suala hili,bado inasisitizwa kwamba kampuni ya TPI Ltd iliiuzia Bohari  ya Dawa (MSD) dawa bandia aina ya TT-VIR 30 toleo Na. 0C.01.85, kwa mujibu wa nyaraka zilizopo.
Tunapenda kusisitiza kwamba, Mhe. Waziri katika hotuba yake hakukanusha kuwa kampuni ya  TPI Ltd iliiuzia MSD dawa bandia bali alieleza kwamba uchunguzi wa awali katika  kiwanda cha kampuni hiyo haukuonesha dawa hiyo ilizalishwa na TPI Ltd  bali vifungashio ni vya TPI Ltd na nyaraka  zinaonesha TPI Ltd kuiuzia MSD dawa hizo bandia.
Aidha, alieleza kuwa vyombo  vya usalama bado vinaendelea kulichunguza suala hilo ili kubaini chanzo na wahusika wakuu wa dawa hizo bandia.
Kwa kuzingatia unyeti wa suala hili, Wizara inatoa wito kwa vyombo vya habari kusubiri hatma ya uchunguzi unaofanywa na vyombo vya usalama na kuepuka  kutoa taarifa ambazo zinaweza kupotosha umma na jitihada kubwa za Serikali  katika kupambana na dawa bandia nchini.



 N. Mwamwaja
MSEMAJI
16 Mei, 2013.
 

Je, Una Habari,Picha,Tangazo,Makala,

Hifadhi blog hii kwenye simu yako ili upate habari zote kwa urahisi zaidi

Facebook Blogger Plugin by Kibonajoro
http://www.facebook.com/kibonajoro

Post a Comment

 
Top