
Kumekuwa na Taarifa potofu zinazosambazwa na baadhi ya
watu katika mitandao ya kijamii ya kuwa “Mwanasheria
Mkuu Zanzibar Othman Masoud Othman amekamatwa
baada ya kupiga kura ya hapana Bungeni leo”.
Tunapenda kuutarifu Umma wa Watanzania kuwa, taarifa
hizo sio sahihi na ni porojo zenye kutaka kuleta hisia potofu
kwa wananchi kuhusu kiongozi huyo.
Ukweli wa Jambo hili ni kuwa Mhe. Othman Masoud
Othman ametekeleza haki yake ya Kidemokrasia ya kupigia
kura Rasimu ya Katiba inayopendekeza katika Bunge
Maalum leo. Ambapo katika kura alizopiga, ameweza
kuzikubali baadhi Ibara na kuzikataa ibara nyingine katika
rasimu ya Katiba inayopendekezwa.
Pengine hatua hiyo ya kuzikataa baadhi ya Ibara,
haikuwafurahisha baadhi ya Wajumbe na hivyo kuleta
majibishano ndani ya Bunge Maalum wakilalamikia uamuzi
wake huo.
Kutokana na hofu hiyo ya baadhi ya Wajumbe kuanza
kupinga uamuzi wake huo ndani ya Bunge, Ofisi ya Bunge
Maalum kama ilivyokawaida kwa kila mjumbe, imeweza
kumpatia Ulinzi Maalum wakati akitoka Bungeni hadi
alipoondoka katika viwanja vya Bunge ili asiweze
kubugudhiwa kwa namna yoyote ile kutokana na uamuzi
wake huo.
Suala hili limechukuliwa kipropaganda na kuanza kueneza
uongo katika mitandao ya kijamii kuwa Mhe. Othman
amekamatwa baada ya kupiga kura ya hapana.
Tunapenda kuwahakikishia Watanzania wote kuwa Mhe.
Othman hajakamatwa bali alipewa ulinzi katika Maeneo ya
Bunge Maalum jambo ambalo hufanyika kwa kila mjumbe
ambaye kwa namna moja ama nyingine itaonekana kuna
dalili za kubugudhiwa katika Maeneo ya Bunge kutokana na
uamuzi au kitendo alichofanya.
Na kutokana na hali ilivyo,
ulinzi wake umeimarishwa pia mahali alipo kwa hivi sasa
mpaka atakapomaliza kazi yake hapa Dodoma.
Kanuni za Bunge Maalum zimempa madaraka Katibu wa
Bunge Maalum kusimamia masuala yote ya Ulinzi na
Usalama kwa Wajumbe na Maeneo yote ya Bunge Maalum.
Imetolewa na Idara ya Habari
Ofisi ya Bunge Maalum
1 Oktoba, 2104
Facebook Blogger Plugin by Kibonajoro






Post a Comment
Post a Comment