![]() |
| Mti wa Mwembe uliopo kati ya Shule ya Msingi Uhuru na Shule ya Msingi Muungano, ambao umegharimu maisha ya Mwanafunzi huku mwingine akilazwa katika Hospitali ya Maweni kwa matibabu. |
Mwanafunzi wa Darasa la Tatu katika Shule ya Msingi Uhuru iliyoko Manispaa ya Kigoma Ujiji, amefariki papo hapo huku mwanafunzi mwingine pia wa darasa hilo akivunjika vibaya mguu na mkono wa kulia baada ya wote wawili kuanguka kutoka juu ya mti wa mwembe.
Tukio hilo lilitokea jana majira ya saa nne asubuhi katika eneo la shule ya msingi Uhuru wakati wanafunzi hao na wengine wakiwa katika kipindi cha mapumziko.
Wanafunzi wengine walioshuhudia tukio hilo walisema wenzao walipanda juu ya mti wa mwembe kwa nia ya kutaka kuchuma maembe ambapo walidandia moja ya matawi ya mti huo ambalo lilizidiwa uzito na kukatika na wao kuporomoka nalo mpaka chini.
“Tulikuwa hapa wote tunacheza wakati wa mapumziko halafu wenyewe wakapanda juu ya mwembe kuchuma maembe na walivofika juu mmoja akasema: “oyaaa, tutaanguka na tukianguka hapa tutakufa,”alisema Rajabu Mhina, mwanafunzi katika shule ya msingi Muungano ambayo ni shule pacha na shule ya Uhuru.
Alisema muda kidogo ghafla wakasikia wenzao wanaanguka kutoka juu ya mwembe.
Jeshi la Polisi Mkoani Kigoma limethibitisha kutokea kwa tukio hilo ambapo Kamanda wa Polisi ACP Jafari Mohamed aliwataja wanafunzi hao kuwa ni Hamim Musa aliyefariki papo hapo baada ya kupasuka kichwa na Baraka Ramadhani aliyelazwa hospitali ya Maweni wote wakiwa na umri wa miaka 11 na wakazi wa Mwanga Shaurimoyo, Manispaa ya Kigoma Ujiji.
Credit by..@kigomapressclub
Facebook Blogger Plugin by Kibonajoro







Post a Comment
Post a Comment