Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This
Jeshi la Pilisi mkoani Kigoma limekamata waganga wa jadi 22 ikiwa ni katika harakati za kupambana na vitendo vya mauaji ya Walemavu wa Ngozi (Albino) vinavyosababishwa na imani za kishirikina.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Kamanda wa Polisi mkoani Kigoma, Kamishina Msaidizi, Japhari Muhamed, alisema kuwa ukamataji huo ulifanyika katika Wilaya nne za mkoa huo ikiwemo wilaya ya Kigoma mjini, Buhigwe, Kasulu na Wilaya ya Kipolisi Manyovu ambapo wanatuhumiwa kwa kufanya shughuli zao bila vibali na kufanya kazi ya kupiga ramli chonganishi zinazopelekea mauaji ya Albino.

Kamanda alisema kuwa licha ya kutokuwepo kwa matukio ya mauaji ya Albino mkoani hapa ila kutokana na kukithiri kwa matukio hayo  katika mikoa mingine nchini, nao wanachukua hatua za kuthibiti vitendo hivyo ili kuhakikisha usalama wa watu wenye ulemavu wa ngozi.

“Mara ya Mwisho kutokea kwa mauaji haya mkoani hapa ilikuwa mwezi wa nne mwaka 2010, ambapo mtoto wa miaka minne aliuwawa ila kesi hiyo ilishighurikiwa kwa mujibu wa sheria” alisema.
Alisema kuwa, moja ya hatua wanazochukua kama jeshi la Polisi ni kuwakamata waganga wa jadi wanaopiga ramli chonganishi ambazo tafiti zinaonyesha ndizo zinazochochea mauaji ya Albino.
“Wale wauaji sio waganga ila wanaua kwa kutekeleza melekezo ya waganga, kwamba ili dawa ifanye kazi ipasavyo kunatakiwa kipatikane kiungo cha Albino hivyo muhusika anakwenda kuua ili apate kiungo hicho” alisema Kamanda
Aidha Kamanda  aliwataja majina waganga waliokamatwa kuwa ni Fikiri Kadola (35), Hamisi Ndegeya (44), Gwizima Fwankyiye (72), Ambrose Nyamtondo (44), Eliud Kitumbu (44) Matesa Mbata (35), Focus Kitulanya (54), Athumani Nguvumali (35), Elias Lazaro (34), Emmanuel Seth,  Kassimu Miyandaza (72), Thabiti Kassim (35), Bakari Nchabironda (50), Jitihadi Juma (56), Nikodem Alex (44), Yoram Nyamwihala (55), Saidi Bahezwa (70) Andrea Issaya (37), Sulvin Samson (42), Samweli Makafi (45), Hamis Ntihabosa (58) na Idrisa Rajabu.

Aliongeza  kuwa, sanjari na kuwakamata waganga hao walikamata vifaa mbalimbali wanavyotumia katika shughuri zao vikiwemo, Ngozi za wanyama mbalimbali, Pembe za Wanyama Pori,  tunguri, kitambaa cheupe na cheusi, mikia ya Wanyama Pori, vibuyu, mabaki ya ndege aliyekauswa, Shanga na dawa za asili.

“Msako wa kukamata waganga hawa tumeufanya ndani ya mwezi huu wa tatu na tunaendelea kukamilisha uchunguzi na baada ya kukamilika wote watafikishwa mahakamani ili kujibu mashitaka yao” alisema.

Hata hivyo kamanda alisema kuwa msako dhidi ya waganga wa jadi wanaojihusisha na shughuri hizo kinyume na sheria unaendelea pia aliwataka wananchi kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa zinzotishia usalama wa Albino ili kukomesha mauaji ya Walemavu hao wa ngozi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wanganga hao akiwemo Emmanuel Seth, Sulvin Samson na Hamisi Ntihabosa walisema wao wanajishughulisha na kutibu watu wenye magonjwa yaliyoshindikana Hospitali na hutibu magonjwa yanayojulikana mara baada ya mgonjwa kupimwa.

Je, Una Habari,Picha,Tangazo,Makala,

Hifadhi blog hii kwenye simu yako ili upate habari zote kwa urahisi zaidi

Facebook Blogger Plugin by Kibonajoro
http://www.facebook.com/kibonajoro

Post a Comment

 
Top