Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga Justus Kamugisha |
Katika hali isiyokuwa ya kawaida wakazi wa kata ya Masekelo na Ndala katika manispaa ya Shinyanga juzi walilazimika kususia mazishi ya Benadetha Steven(35)mkazi wa mtaa wa Mapinduzi katika kata ya Ndala manispaa ya Shinyanga baada ya wana ndugu kushinikiza kufanya vitendo vya kimila makaburini ikiwemo kuupasua mwili wa marehemu kabla ya kuzikwa.
Tukio hilo limetokea juzi mchana katika Makaburi ya Masekelo katika manispaa ya Shinyanga wakati wa mazishi ya mwanamke huyo anayedaiwa kufariki dunia tarehe 1,Januari 2015,katika hospitali ya mkoa wa Shinyanga wakati akipatiwa matibabu baada ya kuugua muda mrefu akisumbuliwa na uvimbe tumboni.
MASHUHUDA WAZUNGUMZA
Mashuhuda wa tukio hilo walisema ndugu wa mwanamke huyo anayetokea wilaya ya Musoma mkoani Mara (Mkurya) walikuwa wanataka ndugu yao apasuliwe tumbo wafanye mambo ya kimila makaburini lakini uongozi wa eneo husika ukasema utaratibu huo ni vyema ungefanyika hospitalini badala ya hadharani watu wakishuhudia.
Walisema waombolezaji waliwaomba ndugu wa marehemu wakamfanyie mambo ya kimila ndugu yao hospitalini badala ya kufanya mambo hayo hadharani.
MGOGORO ULIVYOANZA
“Mgogoro ulianzia nyumbani hata kabla ya kwenda makaburini,ndugu walionekana kuelewa wakatulia na wakati mazishi yanaendelea ndipo ndugu mmoja wa marehemu akaingia kaburini,akiwa amevaa mipira ya mkononi,akiwa na wembe na boksi dogo lililokuwa na kifaranga cha kuku na kuzuia waombolezaji wasitupie udongo kaburini”,alieleza Malunde1 blog mmoja wa mashuhuda aliyejitambulisha kwa jina la Sijali Jumanne.
HALI TETE MAKABURINI
"Ndugu huyo wa marehemu aliingia kaburini baada ya mchungaji kumaliza ibada ya mazishi na kuruhusu mwili wa marehemu ufukiwe,ndipo akaanza kuuchana kwa wembe,akachinja kuku,kisha kumwagia damu marehemu na kumwingiza kuku huyo kwenye tumbo la marehemu,akafunika jeneza na ndugu wakaendelea na mazishi”,aliongeza Jumanne.
Shuhuda huyo alisema kitendo cha ndugu wa marehemu kung'ang'ania kufanya mambo yao ya kimila tena hadharani,kiliwakera wananchi wakaamua kutoka makaburini,na jeshi la polisi likafika eneo la tukio na kuwakamata ndugu wote wa marehemu.
Jumanne aliongeza kuwa ndugu wa marehemu waliamua kufanya hivyo wakiamini kuwa wanaondoa mkosi ili kifo kama hicho kinachotokana na uvimbe tumboni kisitokee tena kwenye ukoo wao.
KIONGOZI WA MTAA ANENA
Mwenyekiti wa mtaa wa Mapinduzi Ayubu Daniel alikiri kuwepo kwa tukio na kuongeza kuwa askari polisi walifika eneo la tukio na kuwakamata ndugu wa marehemu na baadaye kuwaachia kisha mazishi kuendelea siku hiyo jioni.
“Walipokamatwa na polisi walisema ndugu wa marehemu walidai wanafanya mambo ya mila na kwamba mwili wa marehemu tayari ulikuwa umefanyiwa uchunguzi na madaktari hivyo wakaruhusiwa kuzika mwili huo japokuwa mwitikio wa wananchi ulikuwa mdogo sana”,aliongeza mwenyekiti huyo wa mtaa wa Mapinduzi.
Hata hivyo Afisa mtendaji wa kata ya Ndala Dickson Venance aliiambia Malunde1 blog kuwa siku moja kabla ya mazishi kulikuwa na mgogoro juu ya mazishi ya mwanamke huyo ambaye aliolewa na Njunju Maulid mkazi wa Shinyanga bila kulipiwa mahari hivyo ndugu wa marehemu walikataa mwili wake kuzikwa kutokana na mila zao vinginevyo wapasue mwili wakazike kwao mkoani Mara endapo hawatalipwa shilingi milioni moja.
“Kabla ya mazishi,nilisuluhisha mgogoro,ndugu wa marehemu walikuwa wanataka mahari ya shilingi milioni 1,kukawa na mvutano,wakakubaliana shilingi laki 1, ndugu wa mwanamme wakachangishana,wakakubalina kuzika,sikuwepo wakati wa mazishi lakini nashangaa imekuwaje”,alisema afisa mtendaji huyo.
JESHI LA POLISI WANASEMAJE
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, Justus Kamugisha alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba wanandugu waliohusika walikamatwa na kuhojiwa kwa muda na ilipobaika ni mambo ya kimila waliachiwa huru na kuruhusiwa kuendelea na shughuli za mazishi.
Credit Malunde1-Shinyanga
Facebook Blogger Plugin by Kibonajoro
Post a Comment
Post a Comment