Kelele za
vilio jana zilisimamisha kwa muda shughuli katika Wodi ya Wanawake ya
Hospitali ya Mwananyamala, Dar es Salaam baada ya mama mzazi wa
msichana, Yusta Lucas (20) anayedaiwa kuteswa kwa kung’atwa na kuchomwa
kwa pasi mwili mzima kumwona mwanawe kwa mara ya kwanza.
Zilikuwa
dakika 10 ngumu kwa mama huyo, Modesta Simon kuamini hali aliyomkuta
mwanaye aliyelazwa hospitali hapo kuuguza majeraha kutokana na kufanyiwa
ukatili na tajiri yake Amina Maige.
Mwanamke
huyo anashikiliwa katika Kituo cha polisi Oysterbay kwa tuhumu hizo na
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni Thobias Edoyeka alisema leo
atafikishwa mahakamani... “Bado sijafahamu kama atapelekwa ama Kisutu au
Kinondoni.”
Mara
baada ya mama huyo kuingia katika wodi hiyo, Yusta aliyekuwa ameketi
kitandani aliruka na kumkimbilia mlangoni na kilichofuata ni vilio.
Akizungumza
huku akitokwa na machozi, Modesta alisema: “Jamani Amina kweli
amekufanya hivi, kila nikiuliza wananiambia hujambo kumbe umeharibika
hivi...”
Alisema habari za mateso na kulazwa kwa mwanaye alizipata kutoka kwa ndugu yake anayeishi Arusha.
“Alhamisi
nilipata simu kutoa kwa ndugu yangu Marieta Shitindi yeye anakaa
Arusha, akaniambia ameona kwenye Mwananchi na runinga kwamba Yusta
amelazwa baada ya kupigwa na Amina ndipo nikafunga safari kutoka Tabora
kuja kuhakikisha.
Amina ni
mtoto wa mjomba wangu kabisa na sikuwahi kuambiwa chochote, niliamini
wanaishi vizuri na sikudhani kama anaweza kulifanya jambo hili.”
Modesta
alisema awali alikuwa na mawasiliano na mwanaye kupitia simu ya mama
yake Amina ambaye wanaishi karibu, lakini hivi karibuni alianza kupata
wasiwasi baada ya kila alipohitaji kuongea naye alipatiwa sababu hivyo
akaomba Yusta kurudishwa na aliahidiwa angepelekwa mwezi huu.
“Aliniahidi
mwezi huu atamleta Yusta nyumbani alisema anataka muda amnunulie na
cherehani ili akija apate shughuli ya kufanya...” alisema.
Ofisa
Muuguzi katika wodi aliyolazwa Yusta, Erica Massawe alisema hali ya
binti huyo imeimarika na alisharuhusiwa kutoka tangu Ijumaa iliyopita na
kwamba wanasubiri maelekezo ya Polisi na Ustawi wa Jamii kwani ndiyo
wahusika wakuu.
Chanzo:Mwananchi
Facebook Blogger Plugin by Kibonajoro
Post a Comment
Post a Comment