![]() |
| Shekhe Ponda Issa Ponda akisindikizwa na askari mahakamani. |
Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Mkoa wa
Morogoro jana imeshindwa kuanza kusikiliza kesi ya Katibu wa Jumuiya ya
Waislamu Tanzania, Shehe Ponda Issa Ponda.
Kesi hiyo haikuanza kusikilizwa,
kutokana na jalada halisi kutorejeshwa kwenye mahakama hiyo kutoka
Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam.
Pia haikusikilizwa licha ya upande wa Mashikata, kukamilisha upelelezi na mashahidi wake.
Ponda alifikishwa jana saa 3 asubuhi
mahakamani akiwa chini ya ulinzi wa Polisi. Kulikuwa na baadhi ya
wafuasi wake, ambao hawakupata fursa ya kuingia mahakamani.
Hakimu Mkazi Mwandamizi, Mary Moyo
anayesikiliza kesi hiyo, alitumia dakika 21 kusikiliza hoja za pande
mbili za utetezi na ya mashitaka.
Kabla ya kuahirisha kesi hiyo hadi Aprili
16, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa, Hakimu alimuuliza juu ya kukosekana
awali kwa mawakili wake kwenye chumba cha mahakama.
Ponda alisema hakuwa na mawasiliano nao
juu ya kutohudhuria. Hata hivyo, baadaye aliwasili mmoja wa mawakili
wake wa utetezi, Bartholomew Tarimo, aliyemwomba radhi hakimu kwa
kuchelewa wakati akiwa ameshaanza kusikiliza maelezo ya upande wa
mashitaka.
Aidha, wakili Tarimo alidai mahakamani
kwamba amewasiliana na Wakili mwenzake, Juma Nassoro, akamwambia licha
ya ombi la Ponda la mapitio kutupwa na Mahakama Kuu Kanda ya Dar es
Salaam, wamewasilisha ombi lingine Mahakama Kuu.
Kwa mujibu wa Tarimo, wanataka kurejewa
rufaa inayohusu uamuzi wa Mahakama ya Kisutu, Dar es Salaam, kuhusu
shitaka namba moja katika kesi hiyo.
Wakili huyo wa utetezi aliomba kesi ipangwe tarehe nyingine, ikisubiri uamuzi wa Mahakama Kuu.
Wakili wa Serikali aliomba hakimu
asizingatie hoja za Wakili Tarimo, kwa vile kumbukumbu zake zinaonesha
si wakili wa Shehe Ponda, kutokana na kumkataa siku za nyuma.
Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama hiyo,
alimhoji Ponda ataje majina ya mawakili wanaomtetea, akajibu ni
watatu. Alimtaja Tarimo, Juma Nassoro na Yahya Njama.
Upande wa Mashitaka ulidai uko tayari
kuanza kusikiliza kesi hiyo kwa vile umekamilisha upelelezi na
ushahidi. Ulidai upande wa utetezi, unaleta hoja zisizo za msingi kwenye
kesi hiyo, zinazolenga kuchelewesha kwa makusudi.
Hakimu alisema pamoja na ombi la Ponda
kugonga mwamba Mahakama Kuu, jalada halisi la kesi hiyo halijarudishwa
kwake hivyo asingeweza kuendelea na shauri hilo. Mshitakiwa amerejeshwa
rumande hadi Aprili 16 mwaka huu, itakapotajwa tena.
Shehe Ponda alifunguliwa kesi namba
128/2013 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoa wa Morogoro, akikabiliwa
na mashitaka matatu aliyodaiwa kutenda Agosti 10 mwaka jana eneo la
Kiwanja cha Ndege, Manispaa ya Morogoro
Facebook Blogger Plugin by Kibonajoro








Post a Comment
Post a Comment