![]() |
| Jaji Joseph Warioba (wa pili kutoka kulia). |
Tume ya Mabadiliko ya Katiba haikufukuzwa kazi, isipokuwa siku ya ukomo iliwekwa kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.
Ikulu imesisitiza kuwa haikuwa na madaraka wala mamlaka, kuibadilisha.
Aidha, Ikulu imeanika viwango vya posho,
ambavyo wajumbe wa tume hiyo, walikuwa wakilipwa vya kati ya Sh 100,000
na Sh 500,000 kwa siku.
Imesema wanaodhani Serikali ina uwezo wa kulipa kila mjumbe kiinua mgongo cha Sh. milioni 200, wanajidanganya.
Hayo yamo kwenye Taarifa iliyotolewa jana na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu jana Dar es Salaam.
Ilikuwa ikifafanua madai mbalimbali,
yaliyotolewa na magazeti mawili tofauti ya jana; moja likimnukuu
Mwenyekiti wa Tume, Jaji Joseph Warioba akidai Ikulu imewatupia
virago.
Gazeti lingine lilikuwa na habari chini
ya kichwa : 'Bilioni 6 kuipoza Tume ya Warioba' , ikimkariri mjumbe
mmoja wa Tume hiyo, ambaye hakutajwa jina. Mjumbe huyo alidai tume hiyo
inatarajia kupewa Sh bilioni sita, ikiwa ni kiinua mgongo, ambapo kila
mjumbe atapata Sh. milioni 200.
Katika taarifa hiyo, Ikulu ilisema tangu
mwanzo wa mchakato mzima wa Katiba Mpya na utendaji kazi wa Tume hiyo
iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba, hapakupata kuwepo shaka kuhusu
siku ya tume kumaliza kazi zake.
"Mwenyekiti wa Tume, wajumbe wote wa
Tume, Sekretarieti ya Tume na Watanzania wote waliijua fika siku ya
mwisho ya tume kukamilisha shughuli zake. Kwa mtu kujitia ameisahau siku
hiyo leo ni kiwango cha juu sana cha unafiki," ilisema sehemu ya
taarifa hiyo.
Taarifa hiyo ya ikulu, inatokana na
habari iliyochapishwa jana kwenye gazeti la Raia Mwema, ikimnukuu Jaji
Warioba akidai kuwa tume ilifukuzwa kazi kwa maana kwamba haikupewa
muda wa kuandaa na kuwasilisha nyaraka.
Habari hiyo, ilimnukuu Jaji Warioba akidai kwamba wajumbe wa Tume hiyo, waliporwa magari ambayo yamewekwa Ikulu.
Pia, habari hiyo ilidai Tume hiyo
inatarajiwa kupewa Sh.bilioni sita ikiwa ni kiinua mgongo ambacho kila
mjumbe atapata kiasi cha Sh. milioni 200.
Katika ufafanuzi huo, Ikulu ilieleza kuwa
moja ya mijadala mikali ya awali kuhusu mchakato wa Katiba Mpya,
ulihusu lini Tume ya Mabadiliko ya Katiba imalize muda wake.
"Wengine wakitaka Tume imalize muda wake
baada ya kukabidhi ripoti ya Tume na Rasimu ya Katiba, wengine wakitaka
Tume imalize muda wake baada ya Mwenyekiti wake kuwasilisha Rasimu yake
Bungeni na hata wengine wakitaka wajumbe wa Tume wawe sehemu ya Bunge
Maalum la Katiba."
Hatimaye, ilikubaliwa shughuli za tume
zingefikia ukomo wake baada ya Mwenyekiti wake kuwasilisha Rasimu ya
Katiba kwenye Bunge Maalumu la Katiba.
Baada ya Jaji Warioba kuwasilisha rasimu
katika Bunge Maalum la Katiba, Machi 18, mwaka huu, siku iliyofuata
kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Rais alitia saini tangazo
la Serikali la kuvunja tume hiyo lilichapishwa kwenye gazeti la
Serikali, Machi 21.
"Siku hiyo ya mwisho iliwekwa kwa mujibu
wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, na Ikulu haikuwa na madaraka wala
mamlaka yoyote kubadilisha tarehe hiyo. Hivyo, madai ya Ikulu kuitupia
virago Tume ya Mabadiliko ya Katiba hayana msingi wowote na ni jambo la
kutunga tu," ilisema taarifa.
Ilifafanuliwa kuwa tangu Jaji Warioba
alipokabidhi Ripoti ya Tume na Rasimu ya Katiba kwa Rais, Jakaya
Kikwete na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, Desemba 30, 2014,
jijini Dar es Salaam, Sekretarieti ya Tume ilitakiwa kuandaa ripoti ya
makabidhiano.
"Kwa maana hiyo, tokea Desemba 30, mwaka
jana, kupitia miezi ya Januari, Februari mpaka Machi 18, mwaka huu,
Sekretariati ilikuwa na muda wa siku 77, zaidi ya miezi unusu, Ékatika
muda wote huo, ilikuwa inafanya nini badala ya kuandaa ripoti ya
makabidhiano na wakati maofisa wake walikuwa wanaendelea kulipwa
mshahara na Serikali? Kwa nini walalamike hadharani leo kwa jambo ambalo
lilikuwa ni la wajibu wao na wakashindwa kulifanya kwa wakati?,"
imehoji.
Ikulu ilikiri wajumbe wa Tume, walitakiwa
kurudisha Ikulu magari, ambayo walikuwa wanatumia kikazi, kwa sababu
kazi ya Tume ilikuwa imemalizika ;na kwamba ilifahamu yalitakiwa
kupelekwa Dodoma kwa matumizi ya shughuli za Bunge Maalumu la Katiba.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Serikali
ilichukua uamuzi magari hayo yapelekwe Dodoma, kwa sababu lisingekuwa
jambo la busara kwa Serikali kutumia fedha za umma, kununua magari
mengine mapya wakati ya Tume bado yanafaa, kufanya kazi na wala hakuna
bajeti ya kufanya manunuzi ya magari mapya.
Ilikiri, "ni kweli magari hayo yako
Ikulu, Dar es Salaam, yakisubiri kukamilika kwa taratibu za kuyapeleka
Bunge Maalum la Katiba mjini Dodoma."
Suala lingine ambalo linadaiwa kupotoshwa
ni kuhusu taarifa kwamba wajumbe wa tume hiyo, walilipwa kiinua mgongo
cha Sh milioni 200 kila mmoja.
Ikulu ilikiri wajumbe wa tume hiyo, kufanya kazi nzuri na kueleza kuwa wanastahili pongezi nyingi za wananchi.
Lakini, ilisema kama wanadhani Serikali ina uwezo wa kumlipa kila mjumbe kiinua mgongo cha Sh. milioni 200, wanajidanganya.
Imefafanuliwa kwamba alichozungumza Rais
Kikwete tangu mwanzo wa mchakato ni kwamba, atafikiria kuwalipa
wajumbe wa tume aina fulani ya kifuta jasho, ambacho kiwango chake
atakiamua yeye na kwa wakati mwafaka kulingana na raslimali za Serikali.
"Mpaka sasa hajafanya uamuzi juu ya jambo hili," ilieleza taarifa hiyo
ya Ikulu.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, ukweli ni
kwamba wajumbe wa Tume walikuwa wanalipwa Sh. 200,000 kama posho ya
vikao kwa siku. Taarifa hiyo ilikanusha kwamba wajumbe hao wa tume
walikuwa wakilipwa Sh 500,000 kwa siku.
Facebook Blogger Plugin by Kibonajoro








Post a Comment
Post a Comment