Headlines News :
KIGUGUMIZI cha serikali ya Rais Jakaya Kikwete katika kuchukua
uamuzi mgumu kwenye masuala mazito kimemwibua Waziri Mkuu wa zamani,
Edward Lowassa, akisema nchi inakosa viongozi jasiri wenye kusimamia
utekelezaji wa mambo waliyoamua katika sekta mbalimbali.
Edward Lowassa.
Alisema nchi ina tatizo kubwa la uswahili mwingi wa kukaa kutekeleza
kile kinachotakiwa kufanyika kiasi cha kuwafanya kila mtu kuanza
kulalamika.
“Hapa mnaamua bila kutekeleza, watu hawana ujasiri wa kufanya
maamuzi magumu, ni lazima awepo mtu mmoja wa kuamua si wote kulalamika
lalamika.
“Tukishakubaliana mambo ni lazima yafanyike. Ni lazima tuondokane
kuwa nchi ya kulalamika kuanzia kiongozi wa juu mpaka mwananchi,”
alisema.
Lowassa aliyasema hayo jana bungeni wakati Bunge lilipokaa kama
Kamati ya Mipango ili kujadili Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka
2014/16.
Lowasa ambaye ni mbunge wa Monduli (CCM) alisema kuwa ni vema
serikali ingekuwa na mipango michache yenye kutekelezeka na tija kwa
taifa.
Aliongeza kuwa kama angekuwa kiongozi wa serikali angejikita kwenye
vipaumbele vitatu ambavyo ni ajira, Reli ya Kati na elimu kuliko kuwa na
vipaumbele vingi visivyotekelezeka.
Alibainisha kuwa tatizo kubwa linaloifanya serikali ishindwe kufanya
vizuri kwenye maeneo mbalimbali ni kujiwekea vipaumbele vingi huku
rasilimali zake zikiwa chache na wakati mwingine zile zinazopatikana
hazitumiwi vizuri.
“Vipaumbele vingi mno utekelezaji wake ni tatizo, tungechagua
vichache, tukavisimamia na tuvitekeleze. Tukiwa navyo vingi kwa wakati
mmoja hatuwezi kuvitekeleza vyote, tuanze na vichache tukivimaliza
tunavifuata vingine.
Ajira
Alisema kama angekuwa kiongozi wa serikali angeanza na kipengele cha ajira ambacho kinakwenda sambamba na mipango.
“Huwezi kupanga bila kuzungumza habari za ajira, tukiri kuna
Watanzania wengi wamemaliza kidato nne, sita, chuo kikuu, vyuo, darasa
la saba walioko mitaani hawana ajira.
“Tusipowashughulikia, watakula sahani moja na sisi, tusipoangalia
yatatufika yale ya wenzetu ya Afrika Kaskazini, si lazima yatufike
lakini hawa wasio na ajira watakula sahani moja na sisi,” alisema.
Lowassa aliongeza kuwa wanapaswa kuangalia suala la ajira kwa umakini
sana, kwamba inawezekana sana kila mmoja akifanya wajibu wake.
Alibainisha kuwa nchi ya Hispania ilikuwa na tatizo kubwa la ajira
mara baada ya kutokea kwa mdororo wa uchumi duniani lakini walikaa chini
na kuamua kulitafutia ufumbuzi.
“Wale wenzetu waliamua kila mwekezaji anayekwenda kwao sharti kubwa
ni lazima atoe ajira kwa vijana, baada ya miaka miwili walipiga hatua
kubwa sana, lazima tuliangalie suala hilo kwa umakini mkubwa sana,”
alisema.
Lowassa aliwapongeza Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Fatuma Mwasa na Mkuu wa
Wilaya ya Igunga, Elibariki Kingu kwa kuamua kuangalia suala la ajira
kwa vijana.
Alisema viongozi hao wamethubutu kwa kuwachukua vijana waliomaliza
chuo kikuu na kuwapa matrekta na kuwatafutia ardhi ya kilimo ambapo hivi
sasa wanaendesha shughuli zao vizuri.
Aliongeza kuwa Benki ya CRDB nayo imeanza kutoa mikopo kwa vijana
wanaomaliza vyuo vikuu kwa kuchukua vyeti vyao kama dhamana.
“Wizara, watendaji na viongozi mbalimbali kila mtu angetimiza wajibu
wake katika hili jambo nina hakika tatizo la ajira lingepungua kwa kiasi
kikubwa,” alisema.
Elimu
Alisema mjadala wa elimu usipuuzwe kwa kuwa lipo tatizo la msingi katika elimu ya Tanzania na hatua zinazochukuliwa hazitoshi.
Aliongeza kuwa alitegemea ripoti ya tume iliyoundwa na Waziri Mkuu
kuchunguza matatizo ya elimu hapa nchini ingetolewa bungeni na
ikajadiliwa ili wabunge wajue matatizo yaliyopo na namna ya kuyatatua.
“Haitoshi kuchukua wanafunzi wengi kumaliza chuo kikuu wakati akienda
kwenye soko digrii anayoipata haifai, hawezi kupata kazi kwa kuwa aina
ya elimu aliyoipata haimuwezeshi kuajiriwa.
“Wenzetu Ujerumani wanagawa digrii nusu inatokana na ujuzi wa kitu
fulani na nusu iliyobakia inatokana na elimu aliyoipata hivyo kila kundi
hapa lina uhakika wa ajira,” alisema.
Alisema kelele zinazopigwa na wananchi juu ya matatizo ya elimu
zinapaswa zisikilizwe na uitishwe mjadala wa jambo hilo ili Tanzania
isiachwe na jumuiya mbalimbali ikiwemo ile ya Afrika Mashariki.
“Tukiacha mambo haya yaendelee kwenye elimu yetu tutakuwa wababaishaji na tutaachwa katika soko la ajira duniani,” alisema.
Reli ya Kati
Alisema kipaumbele chake kingine ni kuboresha reli ya kati ambayo
itachangia kupunguza uharibifu wa barabara zinazojengwa kwa gharama
kubwa na serikali.
Lowassa alimpongeza Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli kwa jitihada
zake za kusimamia ujenzi wa barabara ambazo hivi sasa zimekuwa
zikiharibika kwa kiwango kikubwa kutokana na magari kupitisha mizigo
mikubwa.
“Maroli yaliyopaswa kusafirishwa kwa treni hivi sasa yanasafirishwa
kwa magari, hapa ni lazima barabara ziharibike, naomba muangalie kwa
haraka sana Reli ya Kati,” alisema.
Lowassa pia alimpongeza Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harisson Mwakyembe,
kwa jitihada za kutafuta ufumbuzi wa foleni za jijini Dar es Salaam
ambazo zinachangia kuzorotesha ukuaji wa uchumi.
“Foleni Dar es Salaam it’s a nightmare (jinamizi), muda tunaokaa
katika foleni ukiujulimsha ni mrefu sana serikali ni lazima mchukue
hatua sasa, si suala la kusubiri,” alisema.
Afrika Mashariki
Lowassa aliitaka serikali kuacha kugombana na marais wa Rwanda, Paul
Kagame, Uhuru Kenyatta (Kenya), Yoweri Museveni (Uganda) ambao wameamua
kushirikiana na Sudan katika masuala mbalimbali.
Asema Tanzania ijielekeze zaidi kuimarisha ushirikiano na Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Watu wa Congo ambako kuna manufaa makubwa zaidi.
Sumaye kufunguka
Wakati huo huo, Waziri Mkuu mstaafu wa Awamu ya Tatu, Frederick
Sumaye, ambaye ni mmoja wa watu wanaotajwa kuutaka urais mwaka 2015, leo
anakutana na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuanika kile
kinachoelezwa kuwa ni mchezo mchafu unaofanywa na mahasimu wake.
Hatua ya kada huyo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), inafuatia tukio la
hivi karibuni akidai kuhujumiwa katika mwaliko aliopewa na vijana wa
asasi isiyo ya kiserikali inayojihusisha kuelimisha jamii kuhusu
usalama na amani (Public Terrorism Awareness Trust Fund and Human
Welfare (PTA-HW).
Asasi hiyo iliandaa tamasha Jumapili iliyopita jijini Dar es Salaam
na kumwalika Sumaye kuwa mgeni rasmi lakini katika mazingira ya
kutatanisha saa chache kabla ya shughuli hiyo iliyofanyika viwanja vya
Mnazi Mmoja kuanza, aliarifiwa kuwa imeahirishwa na kwamba atataarifiwa
tarehe nyingine itakayopangwa.
Hata hivyo, katika hali isiyoelezeka muda mfupi baadaye maandamano ya
vijana hao yaliwasili katika viwanja vya Mnazi Mmoja na kupokewa
na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) kutoka Wilaya ya Bukoba
Vijijini, Nazir Karamagi.
Dalili za waziwazi za mgawanyiko miongoni mwa waandaji
zilijitokeza baada ya kuwasili kwa Karamagi ambaye hakuwa ametarajiwa
na waandaaji pamoja na washiriki wa tamasha hilo.
Kwa muda mrefu sasa Sumaye amekuwa akidai kuhujumiwa na wapinzani
wake wanaomhofia katika mbio za urais mwaka 2015 ambapo katika Uchaguzi
Mkuu wa CCM mwaka jana alidai kuchezewa rafu ya rushwa.
CHANZO NI TANZANIA DAIMA.
Facebook Blogger Plugin by Kibonajoro








Post a Comment
Post a Comment