WAKATI Mbunge wa Kahama, James Lembeli (CCM), akisema kuwa
serikali yoyote yenye dalili za kuelekea kubaya huanza kufungia au
kudhuru vyombo vya habari halafu binadamu, Muungano wa Mabaza ya Habari
Duniani (WAPC) na Shirikisho la Kimataifa la Waandishi wa Habari (IFJ)
wamelaani kitendo hicho.
Kauli hizo zimekuja zikiwa zimepita siku chache tangu serikali
kuyafungia magazeti ya Mwananchi kwa siku 14 na Mtanzania siku 90, kwa
kile kinachodaiwa ni kuchapisha habari za uchochezi.
Akizungumza na Tanzania Daima jana, Lembeli ambaye kitaaluma ni
mwandishi, alisema kuwa serikali yoyote inayotumia mabavu kama hayo,
hapo kuna madhara, na kwamba ni dalili mbaya kwamba inakoelekea siko.
Alisema kuwa amesikitishwa na hatua hiyo ya serikali kuyafungia
magazeti hayo kwa kutumia sheria kandamizi ya magazeti ya mwaka 1976,
wakati vyombo vya habari siku zote ndivyo vimekuwa watetezi wa wanyonge.
Lembeli alifafanua kuwa sababu kama hizo wakati mwingine ndizo
zinawafanya wananchi kukosa imani na serikali yao, hivyo hata wanahabari
wanapodhuriwa wanaihusisha serikali na matukio hayo.
Alisema kuwa kufungia vyombo vya habari si suluhisho la kutofichua
maovu, kwani siku hizi nchi ipo katika teknolojia ya kisasa na kwamba
ukifungia gazeti wanatumia mitandao.
“Ukifungia mitandao ya online, wanatumia kuhabarishana kwa njia za
simu. Ukianza kumuona baba anaziba midomo ya mtoto wake anayehoji na
kudadisi, basi hiyo nyumba ni lazima iwe na matatizo.
“Suluhisho hapo ni kujibu hoja na si kufungia, na kama kuna kosa, basi
baba anatakiwa kuwa wa kwanza kumkanya mtoto kwa njia sahihi badala ya
kufunga mdomo,” alisema.
Kwa mujibu wa Lembeli, sheria ya magazeti ya mwaka 1976, imepitwa na
wakati huku akishangaa sababu za serikali kushindwa kupeleka muswada
bungeni kuifanyia marekebisho.
WAPC, IFJ wacharuka
Muungano wa Mabaraza ya Habari Duniani (WAPC) umeungana na wadau
wengine wa Tanzania na Afrika kupaza sauti kutaka uhuru wa habari na
haki za binadamu kwa kulaani serikali kuyafungia kibabe magazeti mawili
ya kila siku.
Taarifa ya WAPC kupitia kwa Katibu Mkuu Chris Conybeare, ilisema kuwa
matendo hayo ni ya kuchukiza na kwa wale wanaotafuta umaarufu wa
kidemokrasia au kisiasa, watambue kuwa hayo hayawezekani bila kuwapo na
uhuru wa vyombo vya habari na jamii huru.
Alisema kuwa Watanzania wamejitahidi kwa muda mrefu kuwa na jamii
iliyokomaa kidemokrasia. Kwamba huu ni muda mwafaka wa serikali kufanyia
marekebisho au kuondoa sheria ya kibabe ya magazeti ya mwaka 1976 na
ile ya Usalama wa Taifa ya mwaka 1970.
“Sheria hizo zinazuia uhuru wa mawazo unaokuza demokrasia. Uhuru wa
habari ni muhimu kwa demokrasia na katika haki za binadamu kama
ilivyotangazwa na kifungu cha 19 cha Tamko la Umoja wa Mataifa kuhusu
haki za binadamu,” alisema.
Alisema kuwa kuyafungia magazeti hayo ni kukiuka haki za binadamu na uamuzi huo unapaswa kuondolewa haraka.
Nalo Shirikisho la Kimataifa la Waandishi wa Habari (IFJ) limeeleza
kuhusu wasiwasi mkubwa katika hali ya kuzorota kwa uhuru wa habari
nchini kufuatia uamuzi wa serikali kuyafungia magazeti mawili.
“Tuna wasiwasi na umakini wa Serikali ya Tanzania kwa uamuzi wa
kuyafungia magazeti. Kufungia magazeti maana yake ni kuwazuia waandishi
wa habari wasitoe taarifa kwa umma.
“Huu ni ukiukwaji mkubwa wa uhuru wa habari ambao haupaswi kufikiriwa
kuwa umetokea kwa bahati mbaya,” alisema Gabriel Baglo, Mkurugenzi Mkuu
wa shirikisho hilo, akisema Tanzania ni lazima iyafungulie magazeti
hayo.
Alisema kuwa IFJ inaamini kuwa waandishi wa Tanzania wamekomaa
kimaadili, hivyo hawawezi kuandika kinyume cha maadili ya kazi zao za
kila siku.
“IFJ linaona kuwa serikali haiwezi kuficha kitu chochote kutokana na
kujiingiza katika mijadala na waandishi wa habari ili kutengeneza jamii
ya pamoja inayowajibika,” alisema.
Aliongeza kuwa ukweli ni kuwa Tanzania inaendelea kukandamiza uhuru wa
habari wakati nchi nyingine katika Afrika zinajitahidi kutafuta uhuru
wa habari na uhuru wa kutoa mawazo.
CHADEMA yang’aka
Nacho Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimeeleza
kusikitishwa na adhabu hiyo ya kufungiwa kwa magazeti ya Mwananchi na
Mtanzania.
Taarifa ya Kurugenzi ya Mawasilinao ya chama hicho iliyosainiwa na
John Mnyika, ilisema kuwa serikali imeendelea kutumia sheria mbaya na
madaraka vibaya kufanya uamuzi mbaya, kila inapokosa hoja na uwezo wa
kukabiliana na sauti mbadala au maoni kinzani.
“Suala hili limekuwa dhahiri zaidi baada ya serikali kuamua hata
kuanza kuingilia uhuru wa habari na maoni kwenye mitandao ya kompyuta
(online), pia kutishia kulifungia gazeti la Rai, linalotolewa na Kampuni
ya New Habari (2006) Limited, kwa sababu limeanza kuchapishwa kila
siku,” alisema Mnyika katika taarifa hiyo.
Mnyika alisema serikali inajichanganya. Kwamba hiyo ni dalili ya wazi
kuwa uamuzi wake huo ni mwendelezo wa uamuzi wa kibabe, usiofanywa kwa
masilahi ya Watanzania.
“CHADEMA inapinga na itaendelea kupinga kwa kauli na vitendo, hatua
hii ya serikali yenye lengo ovu dhidi ya umma wa Watanzania. Ni suala
linalohitaji tafakuri yetu sote, kwa nini serikali imeamua kuchukua
hatua hii wakati huu ambapo nchi nzima iko kwenye mjadala wa Katiba
Mpya?” alihoji.
Kwa mujibu wa Mnyika, kufungia vyombo vya habari sasa hivi ni jaribio
la kuleta hofu vyombo hivyo visiripoti kwa uhuru mchakato wa katiba
mpya, hasa habari zenye mwelekeo wa kusema ukweli dhidi ya serikali au
watawala wanaotaka kukwamisha na kuharibu mchakato huo.
CREDIT TANZANIA DAIMA.
Facebook Blogger Plugin by Kibonajoro








Post a Comment
Post a Comment