Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Mrwanda anasema: “Kama mchezaji, nimejifunza kutokana na mazingira kupitia maisha wanayoishi wachezaji wengine waliotutangulia, nikakuna kichwa, nikajipanga.” 
In Summary
  • Anaweza kuingiza zaidi ya Sh350,000 za Kitanzania kwa siku sawa na Sh15 milioni kwa mwezi, kupitia vitega uchumi vyake vya biashara anazomiliki Tanzania.

MAISHA yanahitaji kitu gani tena? Ukiwa na akili na ukiitumia vizuri akili yako, utapiga bao la maisha. Hiki ndicho alichokifanya straika Mtanzania, Danny David Mrwanda. Ndio maana marafiki zake huwa wanamtania kwa kusema kuna ‘Mrwanda mmoja tu duniani.’
Si kosa kusema, Mrwanda ni milionea, kutokana na utajiri alionao anaweza kuishi maisha yoyote anayotaka bila hata kucheza soka. Kazi yake ni soka, fedha anazopata kutokana na soka kama usajili, mshahara na posho aliwekeza na sasa ukimtaja Mrwanda unamzungumzia mwanasoka mwenye mali za maana.
Anaweza kuingiza zaidi ya Sh350,000 za Kitanzania kwa siku sawa na Sh15 milioni kwa mwezi, kupitia vitega uchumi vyake vya biashara anazomiliki Tanzania.
Mrwanda alishtuka mapema na kupanga mambo yake, alitunza pesa na kufanya mambo ya maendeleo akiogopa kuumbuka baada ya kustaafu soka kama inavyotokea kwa wachezaji wengi.
Mrwanda anasema: “Kama mchezaji, nimejifunza kutokana na mazingira kupitia maisha wanayoishi wachezaji wengine waliotutangulia, nikakuna kichwa, nikajipanga.” 

Utajiri wake
Maisha anayoishi Mrwanda jijini Dar es Salaam anastahili kuitwa staa na profesheno wa ukweli. Anamiliki nyumba kubwa ya kisasa iliyopo Kisukuru, Tabata, Dar es Salaam. Kwa haraka makadirio ya thamani ya mjengo huo ni Sh 200 milioni.
Anamiliki usafiri wa nguvu aina ya Nissan Murano, gharama yake ni kama Sh60 milioni.  Mbali na hivyo, anavyo viwanja vinne vyote viko jijini Dar es Salaam kati ya hivyo viwili ameshaanza kujenga na shamba la ekari moja lililopo King’azi, Kinyerezi, Dar s Salaam.
“Mpango wangu ni kujenga nyumba za biashara kama hapa (anaonyesha kiwanja kimoja ambacho kipo karibu na nyumba anayoishi hapo Kisukuru), unaona nimeanza kujenga fremu za duka kwanza huku, kule kwingine naangalia kwanza, naweza kujenga nyumba ya kulala wageni au kupangisha.
“Lile shamba kule bado nalima mazao mbalimbali na kufuga tu, ila nina mpango mkubwa hapo baadaye kwa sasa naangalia kwanza upepo ili nifahamu niweke kitu gani kitakachoniingizia kipato,” anasema Mrwanda.
Mbali na ardhi, ukikutana na daladala yoyote kwa nyuma imeandikwa  ‘Mrwanda The Straika’ kwa chini ‘Maximo’ na mbele ‘Royal Prince’  usijiulize mara mbili kutaka kujua ni za nani? Ni mali ya Mrwanda.
Mrwanda ndiye mmiliki wa daladala hizo, anazo nne, mbili zinafanya safari za Mwenge-Kariakoo na nyingine Mwenge-Posta. Kila daladala moja, inapeleka hesabu ya Sh85,000 kwa siku, ukizidisha mara nne idadi ya daladala hizo ni Sh340,000 kwa siku.
“Nimeandika jina la Maximo kwenye daladala hizo kwa ajili ya kumuenzi kocha wangu (Mbrazili Marcio Maximo) kwani yule alikuwa kama mzazi kwangu,” anasema. “Mbali na kutufundisha mpira, alinifundisha mengi, alikuwa mtu wangu wa karibu na rafiki akinielekeza mambo kuhusu maisha.”
Mrwanda alifundishwa na Maximo wakati kocha huyo alipokuwa akiinoa Taifa Stars. Anayo gari nyingine ya thamani kubwa aina ya Prado, ambalo pia amelifanyisha biashara kwa kukodisha, lakini hapo hakutaka kuweka wazi ni kiasi gani cha pesa anachoingiza kupitia biashara ya kukodisha gari lake la thamani kama hilo.
Maisha ya mpira
Mrwanda anasema pamoja na vitega uchumi alivyonavyo, sehemu kubwa ya kipato chake kinategemea soka, lakini hakutaka kuweka wazi kipato anachokipata kutokana na kazi yake hiyo ingawa anasisitiza mambo ni mazuri.
Kwa sasa anacheza nchini Vietnam na msimu uliomalizika, alikuwa anaichezea Thanh Hoa ambayo amemaliza mkataba nayo baada ya Ligi Kuu Vietnam kumalizika.
“Nitarudi Vietnam, lakini si klabu niliyochezea msimu uliopita, kila kitu kinaenda sawa na nitaondoka mwisho wa mwezi huu kwa ajili ya maandalizi ya ligi, maisha ya Vietnam ni mazuri na naishi vile inavyotakiwa, nakaa kwenye nyumba binafsi nimepewa hifadhi na gari ya kutembelea.
“Huwa tunakutana pamoja na kukaa pamoja kambini kwenye hosteli za timu siku moja kabla ya kucheza mechi, baada ya hapo kila mmoja anakwenda kwake, kiujumla maisha ni mazuri,” anasema Mrwanda.
Mrwanda anasisitiza kuwa, kucheza nje ya nchi ni raha na masilahi ni makubwa lakini kunahitaji uvumilivu kwa mara ya kwanza na ukiwa na malengo utafanikiwa.
“Kucheza nje ni heshima na tunapata sana pesa, lakini kuna changamoto nyingi hasa ubaguzi na mengineyo, unapotafuta namba nchi za watu na wenyewe wapo lazima ugumu uwepo,” anasema.
Mrwanda anasema katika pitapita yake kwenye nchi na klabu mbalimbali, amegundua Tanzania kuna vipaji. “Huko tunakutana na mchezaji ana wasifu wa kutisha hasa hawa wa Afrika Magharibi kama Nigeria na Ghana lakini uwanjani hakuna kitu.
“Tatizo la wachezaji wa Tanzania hawajui kutafuta, wanaridhika na umaarufu wa hapahapa, waoga na maisha ya kujaribu, kule unapokwenda unakuwa mwenyewe, hakuna anayekujua ni lazima upambane.
“Kama unasubiri wakala, utasubiri sana kwa sababu wakala anaangalia faida tu, hataki hasara,” anasema Mrwanda, ambaye ameweka wazi anapopata mchongo, safari za majaribio yake hutumia pesa yake mfukoni kwa hesabu za chakula na malazi na anapokwenda huko anapambana kuhakikisha pesa yake haipotei bure hadi anafanikiwa na kuwataka wengine waige mfano.
Historia binafsi
Mrwanda ni baba wa familia, mkewe anaitwa Ruth Mrwanda ni askari polisi amezaa naye watoto wawili ambao ni Prince (5) ambaye ni mwanaume na jina hilo ndiyo limeandikwa mbele kwenye daladala zake na Precious (miezi minne) ni wa kike.
“Kama Mungu akinijalia napenda niwe na watoto wanne na napenda majina yao yaanzie PR kama yalivyo ya hawa wengine,” anafafanua.
Mrwanda, ni Mtanzania mzaliwa wa Mbeya, lakini alisoma Shule ya Msingi Isoka Zambia, kisha akajiunga na Sekondari ya Meta hadi kidato cha nne na alimaliza kidato cha sita, Kasama Boys nchini Zambia.
“Sikuendelea na chuo baada ya majibu kutoka, kutokana na tamaa ya kucheza mpira nikaacha masomo. Kitendo kile kilimuudhi sana baba, yeye alipenda nisome,” anasema.
“Ni mtoto pekee mwanaume hivyo aliamini msingi wangu ni elimu tukatofautiana, aliamini mpira ni kujifurahisha tu na hauwezi kuendesha maisha lakini tulielewana baada ya mwaka alipofuatilia maisha ninayoishi akaona mafanikio yangu,” anafafanua Mrwanda ambaye kwao wamezaliwa watatu.
Dada yake mkubwa, Jeny alifariki na sasa amebaki na mdogo wake, Anna.
Hadi anafanikiwa alianza kuichezea timu yake ya mtaa ya Awimbo mwaka mmoja na baadaye alijiunga na Polisi Mbeya, 44KJ ambayo baadaye ilibadilishwa jina na kuwa Karume Boys, baada ya hapo alijiunga AFC ya Arusha aliyoichezea msimu mmoja na kwenda Simba ambako alichaguliwa kuichezea Taifa Stars.
Timu za nje amecheza Polisi Rwanda kwa miezi minne, Al Tadamun ya Kuwait na Vietnam katika klabu za Dong Tam Long An na Thanh Hoa.
--------Mwanaspoti

Je, Una Habari,Picha,Tangazo,Makala,

Hifadhi blog hii kwenye simu yako ili upate habari zote kwa urahisi zaidi

Facebook Blogger Plugin by Kibonajoro
http://www.facebook.com/kibonajoro

Post a Comment

 
Top