MWENYEKITI wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji mstaafu Joseph
Warioba, amesema Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya
Mabadiliko ya Katiba wa mwaka 2013 uliopitishwa na Bunge hivi karibuni
unalenga kuifuta tume hiyo kabla ya kumaliza muda wake.
Muswada huo ambao ulipitishwa na wabunge wa CCM pamoja na Augustine
Mrema wa TLP (Vunjo), ulisusiwa na wabunge wa CHADEMA, CUF na
NCCR-Mageuzi kutokana na kuchakachuliwa baadhi ya vipengele huku
Zanzibar ikiwa haijashirikishwa.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Jaji
Warioba alisema miongoni mwa vipengele vilivyofanyiwa marekebisho kwenye
sheria hiyo ni kile kinachotaka tume yake ivunjwe baada ya kuanza kwa
Bunge la Katiba.
Hoja za Warioba ndizo hizo zinazopigiwa kelele na vyama hivyo vitatu
pamoja na makundi ya asasi za kiraia huku viongozi wa serikali na Chama
Cha Mapinduzi (CCM), wakiwabeza na kudai muswada huo ulipitia taratibu
zote.
Alisema marekebisho hayo yanakwenda kinyume cha sheria mama iliyounda
tume hiyo ambayo inaweka wazi kwamba majukumu ya tume yatafika ukomo
baada ya kupigwa kura ya maoni.
Kwa mujibu wa Jaji Warioba, uamuzi wa wabunge hao utaleta mkanganyiko
endapo watashindwa kuelewana kwenye baadhi ya vipengele, kwani
hapatakuwa na mtu wa kuwafafanulia, kwa kuwa tayari tume itakuwa
imevunjwa.
“Sheria iliyounda tume hii inasema wazi kwamba ukomo wa tume ni baada
ya wajumbe wa tume hiyo kutoa elimu kwa umma kuhusu kura ya maoni na
mchakato wa kupiga kura hiyo utakapokamilika.
“Wao hawaoni sababu ya sisi kuendelea kuwapo hapa, nawaomba watafakari
kipengele hicho,” alisema Warioba aliyepata kuwa waziri mkuu wa
Tanzania.
Kabla ya kuhitimishwa kwa mkutano wa 12 wa Bunge mjini Dodoma, wabunge
wa upinzani walitoka nje wakisusia kupitishwa kwa mabadiliko ya sheria
hiyo, wakidai kufutwa kwa baadhi ya vipengele vilivyobadilishwa dakika
za mwisho bila kuwahusisha.
Kususa huko wakati kikao kinaendelea kuliambatana na vurugu baada ya
Naibu Spika, Job Ndugai, kuwataka askari wa Bunge kumtoa nje Kiongozi wa
Kambi ya Upinzani, Freeman Mbowe, jambo lililowafanya wabunge wa vyama
hivyo vitatu kutoka wote.
Pamoja na madai hayo, wabunge hao walilalamikia utendaji wa Kamati ya
Bunge inayoshughulikia Katiba na Sheria chini ya uenyekiti wa Mbunge wa
Viti Maalumu, Pindi Chana, kwa kubadili vipengele hivyo kabla ya
kuupitisha bungeni.
Baada ya wabunge wa upinzani kususa, wabunge wachache wa CCM
waliokuwapo ukumbini hapo na Mrema, walipitisha mabadiliko hayo na
kuyapeleka kwa rais ili asaini na kuifanya kuwa sheria.
Nje ya Bunge
Moto uliowashwa nje ya Bunge na viongozi wa upinzani pamoja na
makundi ya asasi za kiraia umebadili upepo kwani kelele za kumtaka Rais
Jakaya Kikwete kutousaini muswada huo zimezidi kuongezeka.
Ni katika hatua hiyo, mawaziri kadhaa, William Lukuvi wa Ofisi ya
Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), Stephen Wasira na Mathias Chikawe
wa Katiba na Sheria, wamekuwa wakiendelea kuwabeza wapinzani.
Hivi karibuni Waziri Chikawe alifikia hatua ya kumtisha Rais Kikwete
akisema kuwa endapo hatausaini muswada huo kuwa sheria atakuwa
ametangaza mgogoro na Bunge.
Pia Wasira naye amenukuriwa akisema kuwa wanaopinga muswada huo
usisainiwe lazima wampe rais sababu za kutofanya hivyo, kwa vile hana,
na kwamba milango ya Ikulu kwa wapinzani hao kujadiliana na mkuu wa nchi
imefungwa.
Matamshi hayo ndiyo yamewaleta pamoja viongozi wa vyama hivyo na
makundi mengine wakizunguka kwa wananchi kuwaeleza karoso zilizomo
kwenye muswada huo ambao CCM inataka kutumia turufu hiyo kuhodhi
mchakato wa Katiba mpya.
Angalizo la Warioba
Mwenyekiti huyo aliwataka wanasiasa kuacha malumbano katika mchakato
wa upatikanaji wa Katiba mpya, huku akikanusha uvumi kwamba baadhi ya
wajumbe wa tume hiyo wametishia kujiuzulu.
Badala yake aliwataka waketi pamoja na kukubaliana kuhusu vipengele
wanavyotofautiana kwenye rasimu hiyo, kisha kuwaeleza wananchi manufaa
ya kuwa na Katiba ya wote.
“Huu si wakati wa Tanzania kutengana, wanasiasa wanapaswa kutumia
fursa walizonazo kukaa pamoja na kushirikiana ili tupate Katiba bora,
hatuwezi kupata Katiba kwa maandamano, mikutano na mivutano baina ya
vyama vya siasa,” alisema.
Kwa mujibu wa jaji huyo, kilichopo kwenye rasimu hiyo ni maoni ya
wananchi, hivyo hakuna haja ya kubadili, bali kuboresha ili kila
Mtanzania anufaike na uwepo wa Katiba hiyo.
Alifafanua kuwa kuna baadhi ya wajumbe wa mabaraza walidiriki
kuwakashifu wajumbe wa tume yake, hasa kutokana na wanasiasa kutoa
matamshi ya kuwalenga wajumbe hao wa tume.
“Hilo limetusikitisha, matamshi hayo yalitolewa kwa lengo la
kuwadhalilisha wajumbe wa tume na kuishushia thamani kazi kubwa
wanayoifanya ndani ya tume,” alisema.
Jaji Warioba alisema pamoja na changamoto hizo, tume ilifanikiwa
kukamilisha mchakato huo ambapo kwa kupitia mikutano 179 ambayo
ilihudhuriwa na wajumbe 19,337 wa mabaraza ya Katiba walipata maoni.
Mbali na hatua hiyo, Jaji Warioba alisema tume imepokea maoni kutoka
kwa makundi, asasi na taasisi mbalimbali 600 kuhusiana na rasimu ya
Katiba mpya.
Alisema baada ya kukusanya maoni hayo, tume inatarajia kuanza mchakato
wa kuchambua ili kuandaa ripoti itakayokuwa na maboresho na kuikabidhi
kwa rais kwa ajili ya kuendelea kwa mchakato mwingine.
“Tumewahoji wawakilishi wa wananchi kutoka sehemu mbalimbali za
Tanzania Bara na Visiwani, zaidi ya vikundi 176 vyenye uwakilishi wa
watu tofauti tulikusanya maoni yao.
“Naamini Watanzania wanataka Katiba inayoheshimu utu wa mtu, umoja na kuvumiliana,” alisisitiza Jaji Warioba.
Facebook Blogger Plugin by Kibonajoro








Post a Comment
Post a Comment