WENGI walitarajia mke wa Rais wa
Marekani, Michelle Robinson Obama alivyowasili Bongo juzi angekuwa
amevaa gauni la kitenge cha wax, lakini sivyo, ‘first lady’ huyo
aliwashangaza wengi baada ya kushuka kwenye Ndege ya Air Force One akiwa
na gauni jepesi tu.
Michelle aliwasili Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Julius Nyerere siku hiyo kwa sababu ya ziara ya siku mbili
ya mume wake ambaye ni Rais wa Marekani, Barak Hussein Obama Jr.
KUMBE MSHONO WA GAUNI UNA JINA
Mara baada ya kukanyaga ardhi ya
Bongo, baadhi ya watu, hasa wadada wa mjini waliokuwepo uwanjani
walisema gauni alilovaa Michelle linajulikana kwa jina la ‘sindirela’
“Ah! Mke wa Obama amevaa gauni la
sindirela jamani, lile gauni ndiyo habari ya mjini kwa sasa. Kumbe na
yeye wamo. Mimi nilijua atapigilia gauni la kitenge cha wax kumbe,”
alisema mwanadada mmoja aliyevaa suruali ya ‘jinzi’ na fulana ya kijani
maarufu kwa jina la ‘form six’.
Katika hali ya kushangaza, mmoja wa
wadada waliokuwa pamoja na huyo aliyelitaja jina gauni hilo alisema
atakata kitambaa kama cha Michelle hata kama kitakuwa cha rangi tofauti
na kushona mshono wa sindirela.
Michelle mwenye mabinti wawili, Malia
na Sasha alionekana ni mwanamke ‘simpo’ kwa vazi hilo na viatu
alivyovaa licha ya kwamba huenda ni vya bei mbaya.
Baadhi ya watu walisema viatu hivyo
havipatikani kokote kwenye maduka ya Kariakoo jijini Dar, labda maduka
ya katikati ya jiji hasa yale ya Mtaa wa Samora.
HALI YA HEWA YAMPA WAKATI MGUMU
Hata hivyo, hali ya hewa ya siku hiyo
ilimpa wakati mgumu Michelle kwani kutokana na ulaini wa kitambaa,
gauni lake kila wakati lilikuwa likiashiria kupeperuka na hivyo kumfanya
awe makini kulithibiti.
AINGIA OFISI ZA WAMA BILA ULINZI WA KWAPANI
Katika hatua nyingine siku hiyo,
baada ya mumewe Obama kutinga ikulu, Michelle alikwenda kwenye Ofisi za
Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (Wama) inayoongozwa na mke wa Rais
Kikwete, Salma Kikwete zilizopo mjini.
First lady huyo alishuka ndani ya
gari lenye rangi nyeusi na vioo vya giza na kuelekea mlango mkubwa wa
ofisi hiyo ambapo mwenyeji wake, mama Salma alikuwa akimsubiri.
Tofauti na inavyokuwa kwa wakubwa
wengine, Michelle alionekana kutembea peke yake (bila ulinzi wa kwapani)
huku walinzi wake wakiwa mbali naye wakiwa wamesimama wakiangalia
pembeni.
Ulinzi wa Kimarekani ni wa kumwacha
kiongozi kuwa mwenyewe bila kumsonga huku walinzi wakiwa mbali
wakiangalia usalama zaidi mbali na alipo anayelindwa.
Waliompokea Michelle kwenye taasisi
hiyo ni pamoja na mke wa Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin William
Mkapa, mama Anna Mkapa na wasaidizi wengine katika taasisi hiyo.
MUMEWE AWA KIVUTIO, ABONGA KISWAHILI
Katika ziara hiyo, Rais Obama alikuwa
kivutio kikubwa baada ya kushuka Bongo hasa kutokana na mwendo wake wa
kuvuta kwa mbali mguu mmoja.
Wabongo waliowahi kufika Marekani na
waliokuwepo uwanja wa ndege siku hiyo walisema mwendo wa Obama hupendwa
kutumiwa na ‘vijana wa mjini’ wa nchi hiyo hususan ‘maniga’.
Sauti yake wakati wa kutoa hotuba
ikulu nayo iliwavutia wengi waliokuwa wakiamini ingebadilika tofauti na
anavyokuwa nchini mwake.
“Kumbe jamaa sauti yake ni hiyohiyo,
ni nene, kwa kweli inavutia kwa rais, mi nilijua ni kwa Marekani tu,”
alisema Mbongo mmoja alipokuwa akiangalia hotuba hiyo kupitia runinga
ambapo pia alimpongeza kwa uwezo wake mkubwa wa kujibu maswali ya
waandishi wa habari.
Kivutio kingine kilichoonekanna kwa Obama ni kitendo cha kuwasalimia mapaparazi kwa Kiswahili kabla hajaanza ‘kuwahubiria.’
Obama pamoja na kuzungumza ‘kimombo’ alisalimia kwa kusema: habari zenu. Alipomaliza hotuba yake alisema: Asante.
Katika kuonesha huenda kiongozi huyo
anakijua vyema Kiswahili hata alipokuwa nchini Afrika Kusini alitumia
neno asante kuwashukuru raia wa nchini hiyo.
AANIKA HISTORIA YA BABA YAKE
Hakuna jambo lililowavutia Wabongo
kama pale Rais Obama aliposema kwamba baba yake (marehemu Obama) alikuwa
Mkenya lakini muda mwingi aliutumia Tanzania licha ya kwamba hakutaja
sehemu aliyokuwa akifikia mzee huyo.
Facebook Blogger Plugin by Kibonajoro
Post a Comment
Post a Comment