Dar
es Salaam. Rais wa Marekani, Barack Obama juzi alikutana na kundi la
wafanyabiashara 20 wakubwa barani Afrika wakiwemo Watanzania watatu
ambao utajiri wao ulitajwa katika jarida la Ventures Africa
linalozungumzia masuala mbalimbali ya uchumi wa Afrika, kuwa ndiyo
matajiri zaidi nchini.
Obama ambaye ni Rais wa 44 wa Marekani
alikutana na wafanyabiashara hao juzi jioni katika Hoteli ya Hyatt
Kilimanjaro na kufanya nao mazungumzo kwa saa 1:23, huku waandishi wa
habari wakipewa ruhusa ya kupiga picha tu.
Jarida hilo lililotolewa mwaka jana
liliwataja wafanyabiashara hao kuwa ni Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya
Bakhresa Group, Said Salim Bakhresa, Gulam Dewji, Rostam Aziz,
Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni ya IPP, Reginald Mengi na Mwanzilishi na
Mwenyekiti Mtendaji wa Tanzania Infotech Investment Group, Ali Mufuruki.
Hata hivyo, juzi wafanyabiashara waliokuwa katika orodha ya kukutana na Rais Obama ni Bakhressa, Mengi na Mufuruki.
Anayeongoza katika orodha hiyo ni Bakhressa
anayemiliki mali na fedha zenye thamani ya Dola za Marekani 620 milioni
sawa na Sh992 bilioni (Dola moja Sh1,600) akifuatiwa na Dewji ambaye
utajiri wake ni Dola 560 milioni (Sh896 bilioni).
Wengine na kiasi cha mali na fedha
wanazomiliki kwenye mabano ni Rostam (Sh672 bilioni- Dola 420 milioni)
Mengi (Sh448bilioni- Dola 280 milioni) na Mufuruki (Sh176 bilioni - Dola
110 milioni).
Mara baada ya kumalizika kwa kikao hicho,
Rais Obama alizungumza tena na wafanyabiashara wengine 170 kutoka Afrika
na Tanzania kwa dakika 17, lakini hakuweka wazi walichozungumza na
wafanyabiashara hao 20.
Wafanyabiashara wengine waliokuwepo katika
kikao hicho ni pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Africa Finance
Corporation, Andwer Alli, Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Maendeleo Afrika,
Don Kaberuka.
Wengine ni Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki (EAC), Dk Richard Sezibera, Mwenyekiti wa Econet, Strive
Masiyiwa, Mkurugenzi Mkuu wa Equity Benki, James Mwangi, Mwenyekiti wa
Export Trading Group, Mahesh Patel.
Mkurugenzi Mkuu wa General Electric, Jay
Ireland, Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Harith, Tshepo Mahloele,
Mwenyekiti wa Heirs Holdings, Tony Elumelu.
Makamu wa Rais wa Kampuni ya Microsoft
Afrika, Ali Faramawy, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Prudential Plc,
Tidjane Thiam, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Standard Chartered, Peter
Sands, Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Symbion Power, Paul Hinks,
Mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Tanjet, Susan Mashibe
pamoja na Mwenyekiti wa Benki ya United Afrika, Phillips Oduoza.
Katika meza kuu Obama alikuwa amekaa pamoja na Mashibe, Mahloele, Masiyiwa na Kalumbu
Facebook Blogger Plugin by Kibonajoro