Na Baraka Mpenja wa Fullshangwe Dar es salaam
Siku
chache baada ya Serikali ya Tanzania kukataa kuziruhusu timu tatu za
Tanzania, Simba , Yanga na Super Falcons ya visiwani Zanzibar kushiriki
michuano ya kombe la Kagame, leo hii Serikali imeziruhusu klabu hizo
kwenda Sudan kushiriki michuano ya Klabu Buingwa Afrika Mashariki na
Kati, Kombe la Kagame.
Naibu
Waziri wa Habari Utamaduni na Michezo, Amos Makalla akiongea na
waandishi wa habari kanda ya kati Dodomo asubuhi ya leo amesema
wameruhusu klabu hizo ziende Sudan baada ya kuhakikishiwa na Serikali ya
nchi hiyo kwamba itatoa ulinzi wa kutosha dhidi ya timu za Tanzania.
Makalla
amesema wameandikiwa barua na Serikali ya Sudan ikiwahakikishia kwamba
timu za Tanzania zitapewa ulinzi mkubwa zisiathirike na machafuko
yanayoedelea Sudan.
Kufuatia tamko la Serikali kuziruhusu klabu hizo sasa ziende Sudan, sasa ni juu yao ya klabu hizo kuamua kwenda au kutokwenda.
Lakini
Katibu wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA),
Mkenya Nicholas Musonye amekwishatishia atazichukulia hatua kali klabu
hizo zisipokwenda.
Juzi
Serikali kupitia Makalla ilitoa tamko la kuzuia klabu za Tanzania
kutokwenda Sudan kutokana na machafuko yanayoendelea nchini humo.
Kufuatia
tamko hilo, jana Yanga, ambao ni mabingwa watetezi kwa miaka miwili
mfululizo, walitangaza kuvunja kambi yao hadi wiki mbili baadaye, wakati
Kombe la Kagame linaanza kutimua vumbi Juni 18, mwaka huu.
Yanga
wamepangwa Kundi C katika michuano hiyo pamoja na Ports ya Djibouti,
Express ya Uganda na Vital ‘O’ ya Burundi, wakati wapinzani wao wa jadi,
Simba SC wamepangwa Kundi A pamoja na wenyeji El-Mereikh, Elman ya
Somalia na APR ya Rwanda.
Katika
michuano hiyo inayotarajiwa kufikia tamati Julai 2, mwaka huu mjini
Khartoum, Sudan, mabingwa wa Kenya, Tusker wamepangwa Kundi B pamoja na
wenyeji wengine, Al-Hilal, Falcons ya Zanzibar, Al Ahly Shandy ya Sudan
na Al-Nasir Juba ya Sudan Kusini.
Yanga
wataanza kampeni zao za kutetea taji hilo Juni 20 kwa kumenyana na
Express, wakati Simba SC itashuka dimbani Juni 21 kufungua dimba na
El-Mereikh, na mechi zote zitachezwa Elfashar.
Facebook Blogger Plugin by Kibonajoro
Post a Comment
Post a Comment