MWENYEKITI wa CHADEMA Freeman Mbowe, amevituhumu vyombo vya dola kuwa
vinawafahamu watu walioshiriki kwenye mlipuko wa bomu uliotokea juzi
katika viwanja vya Soweto kwenye mkutano wa chama hicho.
Mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe
Mbowe, alisema tukio hilo ni la kupangwa na wamegundua risasi za bunduki aina ya SMG na bastola zilitumika mara baada ya mlipuko huo jambo linalozusha hofu na kudidimiza demokrasia ya vyama vingi.
Mbowe, alisema tukio hilo ni la kupangwa na wamegundua risasi za bunduki aina ya SMG na bastola zilitumika mara baada ya mlipuko huo jambo linalozusha hofu na kudidimiza demokrasia ya vyama vingi.
Wakati Mbowe akitoa tuhuma hizo kwa vyombo vya dola, Mkuu wa Jeshi la
Polisi (IGP), Said Mwema ameunda timu itakayoongozwa na makamishna
wawili (Paul Chagonja na Isaya Mungulu), kwenda mkoani Arusha kuongeza
nguvu ya uchunguzi.
Akizungumza na waandishi wa habari jana mkoani hapa, Mbowe alisema
uchunguzi wa awali walioufanya wamebaini tukio hilo ni la kisiasa na
lilipangwa.
Alisema ni vema serikali ikatangaza kuachana na mfumo wa vyama vingi
kuliko kuruhusu mauaji na vurugu katika mikutano ya vyama vya upinzani
vinavyoonekana kutoa wakati mgumu kwa watawala.
Aliongeza kuwa uchunguzi wa awali katika eneo la tukio umebaini bomu lililolipuliwa ni la kiwandani na si la kutengenezwa.
Alisema katika eneo la tukio maganda ya risasi kutoka katika bunduki ya
SMG na bastola yalikutwa hali inayowafanya waamini kuna watu waliamua
kufanya tukio hilo kwa kupanga.
Mbowe alisema risasi hizo pia ni miongoni mwa zilizopigwa kwenye tanki
la mafuta la gari la matangazo la CHADEMA ambapo zililitoboa.
Alibainisha kuwa inavyoonekana wahusika walitaka kuzalisha mlipuko mwingine mkubwa na kuleta maafa makubwa katika mkutano huo.
“Haihitaji uchunguzi wa kwenda mwezini katika suala hili, ni wazi
walipanga kutuua lakini wakaua watu wasiohusika. Waliouawa hawakuwa
katika mpango wao na wamekuwa wahanga kwa niaba yetu.
“Hata kama utaamua kumuua Mbowe au (Godbless) Lema, huwezi kuiua CHADEMA
kwani chama kitabaki, na wanachama wengine wataendeleza harakati za
chama kama kawaida,” alisema.
Wabunge kutohudhuria Bunge
Mbowe alisema kutokana na tukio hilo ambalo limeua watu zaidi ya watatu,
CHADEMA imeamua kulifanya ni la kitaifa na wabunge wake watashiriki
kwenye maombolezo.
Alisema kuanzia leo wabunge wote wa CHADEMA hawatahudhuria vikao vya
Bunge na watajumuika mkoani Arusha hadi misiba yote itakapomalizika.
Alisema wanatarajia kufunga mahema katika eneo la tukio na marehemu wote
wataagwa katika eneo hilo ambapo ibada zote za Kiislamu na Kikristu
zitafanyikia hapo.
IGP aunda timu
Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Mwema ameunda timu ya kuongeza nguvu ya
uchunguzi itakayoongozwa na makamishna wawili ambao ni Paul Chagonja
kutoka idara ya operesheni na Isaya Mngulu kutoka ofisi ya upelelezi
makao makuu.
IGP Mwema alisema baada ya tukio hilo, jeshi hilo lilituma makamishna
wawili kutoka makao makuu kwa ajili ya kuongeza nguvu ya uchunguzi wa
tukio hilo na kwamba wameshaanza kukusanya taarifa mbalimbali
zitakazoweza kusaidia kuwabaini watu waliohusika.
Alisema wameunganisha nguvu na vyombo vingine vya ulinzi na watawasaka
wahalifu hao pamoja na walio nyuma yao kwa kile alichoeleza tukio hilo
linaashiria kushamiri kwa matendo ya kigaidi nchini.
Akizungumzia tuhuma zinazotolewa na wananchi juu ya Jeshi la Polisi
kuwajeruhi watu kwa risasi za moto, IGP Mwema alisema kila taarifa
inafanyiwa kazi kwa umakini na kwamba baada ya uchunguzi watatoa taarifa
kamili kwa umma juu ya kilichotokea jijini Arusha.
Aliwaomba wananchi wenye taarifa za kuweza kumtambua aliyerusha bomu
pamoja na watu walio nyuma yake wajitokeze au wamtumie ujumbe kupitia
simu yake ya mkononi namba 0754 78 55 57 na kwamba uhusika wao utafanywa
kuwa siri.
IGP Mwema pia alisema watachunguza kauli ya Naibu Katibu Mkuu wa Chama
Cha Mapinduzi (CCM) bara, Mwigulu Nchemba aliyowaambia wakazi wa
Kimandolu kuwa wasipoichagua CCM katika uchaguzi wa madiwani wa Jiji la
Arusha ulioahirishwa jana, watakufa.
Mwema alisema watachunguza kauli hiyo baada ya kuulizwa swali la hatua
zilichochukuliwa kabla na baada ya mlipuko huo dhidi ya kauli ya
Nchemba.
Juzi katika mkutano wa kufunga kampeni za udiwani kwa CHADEMA
uliofanyika kwenye viwanja vya Soweto, kitu kinachodhaniwa ni bomu
kilipuka na kuua watu watatu na wengine kujeruhiwa.
Chanzo: Tanzania Daima
Facebook Blogger Plugin by Kibonajoro
Post a Comment
Post a Comment