JUMUIYA ya Afrika Mashariki (EAC), imeiomba Jumuiya ya Ulaya (EU), iipe muda wa miezi mitatu kujua hatima ya wao kusaini Mkataba wa Kiuchumi na Jumuia hiyo (EPA).
Uamuzi huo ulifikiwa jana Ikulu Dar es Salaam na viongozi wa Jumuiya hiyo baada ya kikao cha 17 kilichodumu kwa takribani saa sita.
Akizungumza baada ya kikao hicho, Mwenyekiti wa EAC, Rais John Magufuli alisema kikao hicho kilikuwa na ajenda nne, ila ya EPA ilikuwa ngumu kulingana na uzito wake.
Alitaja ajenda hizo kuwa ni ripoti ya mgogoro wa Burundi, kuingizwa rasmi kwa Sudan Kusini kwene Jumuiya, kupitishwa kwa Naibu Katibu Mkuu wa EAC na EPA.
Rais Magufuli alisema viongozi wote kwa pamoja walikubaliana kupewa muda wa miezi mitatu ili Sekretarieti ya EAC iangalie na kupitia masharti ya EPA kabla ya kusaini ili kila mmoja afaidike.
Hata hivyo nchi ambazo zilishasaini makubaliano hayo kutoka Jumuiya hiyo ni Kenya.
Alisema katika kikao hicho, walibaini mambo 10 ambayo yanapaswa kuangaliwa kabla ya kufikia uamuzi kwa maslahi ya nchi na wananchi.
Mwenyekiti alitaja mambo ya kuangaliwa kuwa ni kwa namna gani nchi za EAC zitafaidika, njia gani itatumika kuzuia bidhaa za kilimo na kulinda wakulima.
Maeneo mengine ni usawa, makusanyo yatokanayo na bidhaa zitakazoingizwa, Burundi itasainije huku ikiwa imewekewa vikwazo na EU, kujitoa kwa Uingereza EU na athari zake, kukosekana kipengele cha kuruhusu nchi zingine kujihusisha na nchi za EAC kibiashara, kukosekana ushuru wa forodha na kipengele cha nchi kujitoa pale inapoona haijaridhika na mkataba.
Rais Magufuli alisema mkataba huo ukisainiwa kwa wakati huu, nchi wanachama zinaweza kuingia kwenye mtego mbaya.
“Tumejadiliana kwa muda mrefu ila mjadala mkubwa ulikuwa suala la EPA ambapo tumekubaliana tupewe miezi mitatu ili tukutane Januari na kutoa uamuzi wa pamoja,” alisema Magufuli.
Alisema Tanzania iko kwenye mkakati wa kujenga viwanda, hivyo ni lazima iwe makini katika kusaini mkataba huo.
Aidha, aliiomba EU kutoiadhibu Kenya kutokana na uamuzi huo kwani nia yao ni nzuri hivyo wapewe nafasi.
Mwenyekiti huyo alisema viongozi wote walikubaliana kuiidhinisha Sudani Kusini kuwa mwanachama wa EAC na Christopher Bazivamo kutoka Rwanda kuwa Naibu Katibu Mkuu Mpya na mapendekezo ya kutatua mgogoro wa Burundi.
Facebook Blogger Plugin by Kibonajoro
Post a Comment
Post a Comment