SAUTI za "Takbir ... Takbir ..." zilitawala katika Mahakama ya Hakimu
Mkazi Kisutu jana baada ya Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu
Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda na wenzake 49 kuachiwa huru katika
kesi iliyokuwa ikiwakabili. Washtakiwa hao waliachiwa huru na Hakimu
Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Victoria Nongwa.
Katika kesi hiyo upande wa Jamhuri uliwakilishwa na Wakili wa Serikali
Mwandamizi, Tumaini Kweka na upande wa utetezi uliwakilishwa na Wakili
Yahya Njama.
Akisoma hukumu Hakimu Nongwa alisema: “Jamhuri
imeshindwa kuthibitisha mashtaka kuanzia shtaka la kwanza, tatu, nne na
la tano kwa washtakiwa wote, katika mashtaka hayo washtakiwa wote
kuanzia wa kwanza hadi 50 hawana hatia.
“Katika shtaka la pili
la kuingia kwa nguvu katika uwanja wa Markaz Chang’ombe, upande wa
mashtaka umeweza kuthibitisha kwamba Ponda aliingia kwa nguvu hivyo
anatiwa hatiani kwa kosa hilo.
“Shtaka la kuingia kwa nguvu
halielezi adhabu inayostahili kutolewa lakini mahakama inaweza kumpa
adhabu ya kifungo cha miaka miwili jela au faini au vyote kwa pamoja.
“Kwa mshtakiwa wa kwanza (Ponda) hakuna kumbukumbu kwamba ni mkosaji wa
makosa mengine… mahakama inazingatia pia mshtakiwa alikaa rumande kwa
muda mrefu kuanzia Oktoba 18 mwaka jana hadi leo hivyo inamwachiwa kwa
masharti.
Alisema mahakama inamwachia Ponda kwa masharti ya
kulinda amani, awe mwenye tabia njema kwa miezi 12 na endapo atashindwa
atarudi mahakamani apewe adhabu nyingine inayostahili.
Ponda
alisaini fomu za kukubali masharti aliyopewa na kuachiwa huru huku
wafuasi waliorundikana nje ya mahakama wakimsubiri kwa ajili ya kumlaki.
Hata hivyo ndoto zao zilizimwa na polisi ambao waliamuru asitoke nje kwa miguu.
“Hakuna usitoke nje…. Gari litaingia humu humu ndani utapanda, “ hayo
yalikuwa maneno ya askari na maofisa usalama waliomzingira Ponda asitoke
nje kwa miguu.
Naye Ponda wakati akitoka nje ya mahakama
alisikika akisema: “Sikuachiwa kwa huruma ya mtu, ilikuwa ni haki yangu,
kuna kesi nyingine nyingi nzito kubwa ambazo Serikali inashindwa
kuzithibitisha.
“Dola inatengeneza kesi nzito hazina ushahidi,
inaharibu mfumo wa usalama, kesi zote hizo zinatokana na mashinikizo ya
siasa, tuache kutengeneza kesi kwa ajili ya masuala ya siasa.”
Gari aina ya BIGHORN yenye rangi nyeusi ilipoingia ndani ya uzio wa
mahakama, Ponda, mkewe na ndugu mmoja waliingia ndani pamoja na maofisa
usalama kwa ajili ya kumsindikiza hadi nyumbani kwake.
Ponda alitoka nje ya mahakama akiwa ndani ya gari ambalo lilikuwa likisindikizwa na magari ya polisi wenye silaha.
Waumini wa Kiislamu ambao walikuwa nje ya uzio wa mahakama waliishia kupunga mikono huku wakisema Takbir…Takbir.
Awali akisoma hukumu hiyo, Hakimu Nongwa alisema upande wa mashtaka
ulikuwa na mashahidi 16 na upande wa utetezi ulikuwa na mashahidi 53.
Alisema watuhumiwa walikuwa wanakabiliwa na mashitaka matano ambayo ni
kula njama, kuingia kwa nguvu uwanja wa Markaz Chang’ombe mali ya
Agritanza Limited na kuuzuia kwa nguvu uwanja huo.
Mengine ni
kuiba vifaa mbalimbali vya ujenzi vyenye thamani zaidi ya Sh milioni 59
wakati mashitaka ya kushawishi waislamu kukusanyika katika uwanja huo
yakimkabili Sheikh Ponda na Salehe Mukadamu.
“Matukio hayo
yalitokea kati ya Oktoba 12 na 16 mwaka jana. Shtaka la kula njama
halijaeleza washtakiwa walikula njama kutenda kosa gani… mahakama
inajiuliza ni kosa gani walikula njama kati ya mashtaka yanayowakabili.
“Katika kesi hii mahakama haijaona hata shahidi mmoja aliyesema jinsi
washtakiwa walivyokula njama, mahakama inaona kosa la kula njama
halijathibitika, inawaachia huru washtakiwa wote,”alisema Nongwa.
Nongwa alisema shtaka la kushawishi halikusema jinsi Ponda na Mukadamu
walivyowashawishi waislamu kukusanyika katika uwanja wa Markaz na hakuna
shahidi aliyetaja watuhumiwa walioshawishiwa hivyo shtaka hilo pia
halijathibitishwa.
Alisema vilevile hakuna ushahidi kwamba washtakiwa wote ni wafuasi wa Sheikh Ponda.
“Shtaka la pili la kuingia kwa nguvu limethibitika bila kuacha shaka
kwamba Sheikh Ponda aliingia katika uwanja huo hivyo anatiwa hatiani.
Washtakiwa wengine wote kuanzia wa pili hadi wa 50 katika shtaka hili
wanaachiwa huru,”alisema.
Hakimu Nongwa alisema shtaka la
kuzuia kwa nguvu uwanja huo halijathibitika kwa sababu hiyo washtakiwa
wote wanaachiwa huru katika shtaka hilo na shtaka la wizi pia
halijathibitika.
Alisema hakuna ushahidi kwamba msikiti wa
muda uliojengwa na akina Sheikh Ponda ulikuwa na thamani ya zaidi ya Sh
milioni 59, sawa na thamani ya mali za Kampuni ya Agritanza Limited.
“Naona shaka kama malighafi yote iliyojenga msikiti wa muda ilikuwa
mali ya Agritanza Limited, mahakama inatia shaka hivyo kosa la wizi
halijathibitika. Washtakiwa wanaachiwa huru kwa shitaka hilo pia.
“Upelelezi katika kesi hii haukufanyika vizuri, ungefanywa vizuri
washtakiwa wote wangeweza kutiwa hatiani kwani ukisikiliza ushahidi wao
unaweza kuhisi kwamba walishiriki lakini mahakama haiwezi kuwatia hatia
kwa vile wenye jukumu la kuthibitisha mashtaka ni Jamhuri,” alisema
Nongwa.
Hakimu Nongwa alisema ni jambo lisilobishaniwa kwamba kipande cha ardhi kinachodaiwa kuwa cha Agritanza Limited kina mgogoro.
BAKWATA walibadilishana na Kampuni ya Agritanza Limited bila waislamu
wengine kuridhia. Mahakama ya Kisutu haina uwezo wa kumaliza mgogoro wa
ardhi hivyo wasioridhika wanatakiwa kufuata taratibu kwa kupeleka madai
yao katika Mahakama ya Ardhi.
Facebook Blogger Plugin by Kibonajoro
Post a Comment
Post a Comment